2014-04-18 12:01:53

Yesu amechagua Njia ya Msalaba!


Njia ya Msalaba ni Ibada ambayo inamwonesha Yesu akiwa katika hatua za mwisho mwisho wa maisha yake kama sehemu ya mchakato wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni njia inayoanza kule kwenye Mlima wa Mizeituni na kuishia Mlimani Golgotha, mahali Yesu aliposulubiwa na hatimaye kujisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti.

Hii ni njia ambayo Roho Mtakatifu amemwandalia Mwana wa Mungu, ikapendwa na Mama Kanisa kama chemchemi ya Sakramenti za Kanisa na mshikamano kwa binadamu. Yerusalemu ni mji ambamo Yesu aliweza kufanya Njia ya Msalaba kwa mara ya kwanza, tukio ambalo waamini wanalirudia wakati wa Kipindi cha Kwaresima, lakini kwa namna ya pekee, Ijumaa kuu. Kuna watakatifu wengi ambao walijitosa kimasomaso kuendeleza Ibada hii katika maisha na utume wa Kanisa, kati yao ni Mtakatifu Bernard wa Clairvaux, Mtakatifu Francisko wa Assis pamoja na Mtakatifu Bonaventura.

Baba Mtakatifu kila mwaka wakati wa Ijumaa kuu anaungana na waamini pamoja na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo. Tangu mwaka 1991 kumekuwepo na tafakari mbali mbali za Njia ya Msalaba zilizoandaliwa na watu kadiri ya matashi ya Baba Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa watumiaji wwa mitandao ya kijamii, Ijumaa kuu anasema, kumfuasa Yesu kwa ukaribu zaidi si rahisi, kwa sababu amechagua barabara ambayo ni Njia ya Msalaba.







All the contents on this site are copyrighted ©.