2014-04-18 15:10:39

Mkesha wa Pasaka 2014


Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anasema, Ibada ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo, Ijumaa kuu inatarajiwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa waamini na mahujaji kutoka ndani na nje ya Italia. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Njia ya Msalaba anatarajiwa kutoa Neno kwa ajili ya kufunga tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo.

Wakati wa Njia ya Msalaba, watu mbali mbali watasaidiana kuubeba kadiri ya tafakari zilivyoandaliwa. Hawa ni watu wenye umri tofauti na kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hali inayoonesha Ukatoliki wa Kanisa. Jambo la msingi ni mateso na mahangaiko makubwa wanayokabiliana nayo watu katika medani mbali mbali za maisha.

Padre Lombardi anasema Ibada ya Njia ya Msalaba inaweza kuchukua muda wa saa 1:15. Ibada ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo itarushwa katika nchi zaidi ya 50 zitakazokuwa zimejiunga kutoka Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV. Katika kesha la Pasaka, Wakatekumeni 10 watabatizwa na Baba Mtakatifu Francisko, kati yao 5 ni kutoka Italia, wengine ni kutoka Bielorussia, Senegal, Lebanon, Ufaransa na Vietnam.

Baba Mtakatifu katika Ibada ya Misa Takatifu, Pasaka ya Bwana, ataadhimisha Ibada ya Misa peke yake na baadaye kutoa salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwenguni, maarufu kama "Urbi et Orbi". Hakutakuwa na salam katika lugha mbali mbali kama ambavyo wengi wamezoea. Maadhimisho ya Pasaka kwa Mwaka 2014 yanavionjo vya kiekumeni anasema Padre Federico Lombardi.







All the contents on this site are copyrighted ©.