2014-04-18 08:32:29

Ijumaa kuu na hatima ya watanzania!


Askofu mkuu Paulo Ruzoka, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, wakati wa Maadhimisho ya Ijumaa kuu anasema, hii ni siku ambayo Mama Kanisa anakumbuka mateso na kifo cha Kristo Msalabani. RealAudioMP3

Ni siku ya majonzi na simanzi inazomwonesha Yesu aliyejisadaka kwa ajili ya wokovu wa walimweng pamoja na kutimiza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni. Lengo lilikuwa ni kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu inayomwonesha Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo kwa wote.

Askofu mkuu Ruzoka anasema hakuna mateso makali zaidi kuliko kutengwa na Mwenyezi Mungu, kwani huku ni sawa na kuishi gizani pasi na mwanga wa imani, matumaini na mapendo. Kwa mateso, kifo na ufufuko, Yesu ameleta mwanga, hali na mwelekeo mpya na hivyo wote wamefanyika kuwa ni watoto wateule wa Mungu. Kumbe, maadhimisho ya Ijumaa kuu ni msingi mkuu wa tumaini la Pasaka, chemchemi ya furaha, amani, upendo na mshikamano.

Huu ni mlango mpya katika maisha ya mwanadamu, kwani Yesu anawakomboa watu kutoka katika giza la kukosa mwanga wa imani na ufahamu na hatimaye kuwakirimia maisha mapya katika haki na ukweli. Ijumaa kuu ni msingi wa tumaini na hatima ya mwanadamu katika mchakato wa kufikia maisha ya uzima wa milele.

Askofu mkuu Ruzoka anasema kwamba, watanzania wako katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya, inayohitaji umakini mkubwa katika kujenga na kuimarisha mshikamano wa kitaifa. Watanzania wanangojea kwa matumaini makubwa kupata Katiba Mpya itakayowawezesha kuondokana na mambo yanayokwenda kinyume cha maisha ya binadamu; mambo ambayo kimsingi yanavuruga: haki, amani na utulivu; kwa kuwajaza watu hofu pamoja na mashaka ya hatima ya maisha yao.

Askofu mkuu Ruzoka anasema, watanzania wanapaswa kujiaminisha kwa Kristo Yesu, ili aweze kuwanusuru katika mambo yote haya. Mchakato wa Katiba Mpya nchini Tanzania unawanyima watu wengi usingizi. Watanzania wanaendelea kujiuliza maswali ya msingi, Je, Tanzania itapata Katiba Mpya itakayofuta machozi na mahangaiko ya watanzania wengi? Je, itakuwa ni Katiba inayoleta: mwanga, mwono, dira na mwelekeo mpya katika medani mbali mbali za maisha ya mtanzania?.

Askofu mkuu Ruzoka anasema, kuandika Katiba Mpya ni kazi nyeti na tete. Kumbe, kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza wabunge wa Bunge Maalum la Katiba kwa njia ya sala na majitoleo, ili kweli Katiba Mpya ambayo ni sheria mama iweze kuwaweka watanzania wote huru; kwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kuheshimu na kuzingatia utawala bora.

Waamini waendelee kuwaombea wabunge kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaangazia akili zao na kuimarisha utashi wao ili waweze kutekeza dhamana hii nyeti kwa ajili ya mafao ya watanzania wengi ili kuwapatia watanzania Katiba Mpya ambayo italinda na kudumisha maendeleo ya sasa na kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.