2014-04-18 10:07:30

Hakuna maendeleo ya kweli pasi na uwepo wa Mungu!


Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa kuu la Costantinopoli katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Pasaka kwa Mwaka 2014 anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika mipango na mikakati yao ya maisha, kwani kwa kuunganika na Mwenyezi Mungu, hapo mwanadamu anaweza kupata uhuru kamili!

Kwa bahati mbaya anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza historia ya maisha ya mwanadamu inaandamwa na uwepo wa giza la kifo, ukosefu wa misingi ya haki, amani na utulivu, badala ya kutawala amani, upendo na mshikamano wa kidugu; bado watu wametawaliwa kwa chuki na uhasama badala ya kutoa nafasi kwa upendo na msamaha wa kweli kujikita katika undani wa mioyo yao. Watu bado wanashahuku ya kutembea katika giza la kifo badala ya kukimbilia mwanga unaoletwa na Yesu Kristo mfufuka.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na matamko mbali mbali yaliyotolewa na viongozi mbali mbli wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utaifa na madhulumu, bado mambo haya yanaendelea kushika kasi ya ajabu kwenye medani mbali mbali za kimataifa, kiasi cha kuhatarisha misingi ya amani, utulivu na mshikamano katika Jumuiya ya Kimataifa.

Inasikitisha kuona kwamba watu wanashindwa kuvumiliana na kuheshimiana kutokana na tofauti zao mbali mbali, ambazo kimsingi zinapaswa kuwa ni utajiri kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ubaguzi wa rangi, nyanyasona madhulumu ya kidini, kisiasa na kikabila yanapata chimbuko lake katika mwelekeo huu wa watu kushindwa kuvumiliana. Historia inaonesha kwamba, hakuna maendeleo ya kweli kwa mwanadamu pasi na uwepo wa Mungu.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema hakuna Jamii yoyote ile inayoweza kujikita katika kasi ya maendeleo ya kweli yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili pasi na uhuru wa kuabudu unaopatikana kwa kukubali na kumpokea Mwenyezi Mungu katika maisha ya mwanadamu. Karne ya ishirini iliyopita, ilishuhudia majanga mbali mbali katika historia ya maisha ya mwanadamu Barani Ulaya na sehemu nyingine za dunia. Kumetokea mauaji ya kimbari kutokana na chuki za kikabila, watu wakapoteza maisha.

Dunia imegeuka kuwa ni tambara bovu linaoongozwa na falsa ya "mwenye nguvu mpishe". Huku ndiko baadhi ya mataifa na watu wenye nguvu na uwezo katika medani mbali mbali za maisha wanataka kuiburuza dunia! Kuna baadhi ya watu wamepoteza dira na moyo wa huruma na mapendo, wamegeuka kuwa ni "wanyama" jambo la kusikitisha sana!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, licha ya patashika na nguo kuchanika zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa njia ya Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, ameleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya mwanadamu, Msalaba sasa umekuwa ni alama inayoonesha hekima na ushindi wa Mungu dhidi ya dhambi ya kifo.

Hakuna binadamu aliyewahi kuteseka kama alivyoteswa Yesu na hatimaye, kufa kifo cha aibu pale juu Msalabani. Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, alijinyenyekesha na kutii hadi mauti ya Msalaba, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.







All the contents on this site are copyrighted ©.