2014-04-17 08:56:18

Busu la usaliti lililofanywa na Yuda Iskarioti!


Kardinali Angelo Comastri mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Siku ya Jumatano, tarehe16 Aprili 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa wafanyakazi wa Vatican kama sehemu ya maandalizi ya Siku kuu ya Pasaka, kwa kufanya tafakari ya kina kuhusu busu la usaliti lililofanywa na Yuda Iskarioti kwa Yesu. Je, ni mambo yepi ambayo waamini wanapaswa kujifunza kutoka kwa Yesu aliyemchagua na kumkabidhi kutunza mkoba kwa ajili mahitaji ya mitume wake!

Kardinali Comastri anasema Yesu anataka kuwafundisha mitume wake kwamba, kila mwamini asipokuwa makini na mwaminifu kwa Yesu na Kanisa lake, anaweza kuwa msaliti mkubwa kiasi cha kuwashangaza watu. Hata katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, bado kuna hatari ya kukutana na kivuli cha Yuda Iskarioti, changamoto kwa kila mwamini ni kuhakikisha kwamba, anakesha na kusali, ili asije akatumbukia katika kivuli cha Yuda na hapo atakiona cha mtema kuni!

Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwahurumia hata watu kama Yuda Iskarioti, jambo la msingi ni kutambua dhambi hii na hivyo kukimbilia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Kwa bahati mbaya, Yuda Iskarioti hakuwa na fadhila ya unyenyekevu wala hakuthubutu kuomba tena huruma na msamaha kutoka kwa Kristo na matokeo yake akatenda dhambi kubwa zaidi ya kujikatia tamaa na huruma ya Mungu.

Kardinali Angelo Comastri anasema, Mwenyezi Mungu anamkirimia kila mwamini nafasi ya kutubu na kumwongokea, kumbe, hakuna sababu ya kujikatia tamaa kwa huruma na upendo wa Mungu, kwani hakuna dhambi ambayo haiwezi kusamehewa mbele ya Mungu. Waamini wajenge ndani mwao moyo wa toba na ari ya kutaka kumwongokea Mungu ili kuanza tena ukurasa mpya wa maisha yao ya kiroho na kiutu!







All the contents on this site are copyrighted ©.