2014-04-16 07:46:24

Upendo wa Kristo unalibidisha Kanisa kuwaonjesha watu imani, matumaini na mapendo!


Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum anasema, upendo wa Kristo unawawajibisha kuwaonjesha watu imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Mshikamano huu wa upendo unajionesha hasa kwa watu ambao wanaogelea katika maafa asilia, vita, umaskini na magonjwa. RealAudioMP3

Hii ndiyo changamoto iliyompeleka Kardinali Sarah kutembelea na kuzindua miradi kadhaa inayogharimiwa na Cor Unum nchini Guatemala.

Kardinali Sarah ana mpango pia wa kutembelea Haiti na Ufilippini, maeneo ambayo yameguwa kwa namna ya pekee na maafa asilia. Upendo wa Kristo unaliwajibisha Kanisa kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kuwainjilisha watu kama alivyofanya Mtakatifu Paulo, kwa njia ya huduma makini kwa watu wanaoteseka kiroho na kimwili. Upendo na mshikamano kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro unapaswa kujionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya vitendo na maisha ya kiroho yanayojikita katika sala na sadaka.

Kanisa linapenda kuonesha kwa vitendo kwamba, daima liko karibu na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kama njia ya kuonesha ushuhuda wa Kiinjili. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia kuwa, maskini wanapaswa kuonjeshwa Injili ya Furaha na kumegewa: amani, huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Akiwa Jimbo Katoliki la Lima nchini Guatemala, Kardinali Sarah amekabidhi nyumba 19 zilizojengwa na Cor Unum baada ya wananchi kukumbwa na mafuriko pamoja na tetemeko la ardhi na hivyo kupelekea makazi ya watu kubomoka, kunako mwaka 2011. Hawa ni watu waliokuwa wamejikatia tamaa kutokana na mateso waliyokuwa wanakabiliana nayo.

Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na Mashirika yake ya Misaada yaliyokuwa yanaratibiwa na Ubalozi wa Vatican nchini Guatemala, yaliweza kukamilisha ujenzi wa nyumba hizi ambazo zimekuwa ni chemchemi ya matumaini mapya kwa familia nyingi nchini humo.

Cor Unum imejenga pia Kikanisa cha Mtakatifu Rosa wa Lima, mahali ambapo waamini wataweza kukutanika kwa ajili ya maadhimisho ya Liturujia na maisha ya Kisakramenti. Hili ni eneo la kukutanikia kwa ajili ya kutajirishana katika maisha ya Kikristo. Ni nyumba zenye hadhi ya maisha ya kifamilia. Ametembelea na kujionea huduma mbali mbali zinazotolewa na Caritas Guatemala, kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, walemavu na kambi ya vijana wasiokuwa na ajira, wanaopewa mafunzo ya ufundi, ili waweze kujiajiri baadaye.

Wananchi wa Guatemala wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwajali maskini katika maisha na utume wake. Wanaendelea kumwombea afya njema ya roho na mwili. Huduma makini kwa maskini ni ushuhuda mkubwa wa Uinjilishaji Mpya. Kardinali Robert Sarah anasema, mwezi Juni atafanya hija ya kichungaji nchini Haiti ili kukabidhi shule kubwa ambamo watoto watapata elimu ya msingi na wanawake watapata kufundishwa ujuzi na maarifa. Akiwa nchini Ufilippini, Kardinali Sarah atakabidhi pia nyumba ya wazee na Kliniki pamoja na baadhi ya majengo yanayohusiana na huduma hizi.

Myumbo wa uchumi kimataifa, umetikisa hata huduma ya upendo inayotolewa na Mama Kanisa, lakini hakuna sababu ya kukata tamaa, bali Kanisa litaendelea kusonga mbele kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.








All the contents on this site are copyrighted ©.