Jitahidini kuwa ni Mapadre wenye mvuto na mashiko kwa ajili ya Watu wa Mungu!
Alhamisi kuu, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya siku ile iliyotangulia kuteswa kwake
Yesu Kristo alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti ya Daraja
Takatifu la Upadre, akaonesha kwa njia ya mfano wa maisha yake, jinsi ya kuwahudumia
watu kwa upendo.
Alhamisi kuu
asubuhi, Kanisa linaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki mafuta
ya Krisma ya Wokovu. Mapadre wanaungana na Maaskofu wao mahalia ili kurudia tena ahadi
zao za Kipadre.
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki Iringa ambaye
pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio
Vatican anabainisha kwamba, kwa Makanisa mengi nchini Tanzania, si rahisi sana kuadhimisha
matukio ya Alhamisi kuu kwa pamoja kutokana na sababu za kijiografia na kichungaji.
Kumbe, kwa Majimbo mengi, Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta ya Krisma
hufanywa mapema, ili kutoa nafasi kwa Mapadre kurudi Parokini kwao, ili kuendelea
na huduma za kichungaji, Juma kuu.
Askofu Ngalalekumtwa anasema kwa namna
ya pekee Siku ya Alhamisi kuu, Mapadre wanaalikwa kumtazama na kumtafakari Yesu Kristo
aliyejitoa kama Mchungaji na Kiongozi, akaonesha uaminifu, utii na upendo usiokuwa
na mipaka kwa waja wake. Uaminifu wa Kristo uwe ni changamoto ya uaminifu wa Mapadre
unaojionesha kwa namna ya pekee katika: upendo, unyofu, unyenyekevu na huruma.
Mapadre
wajitahidi kuwa ni watu wenye mvuto si kwa sababu ya kuwapendeza watu, bali kutokana
na unyofu wa maisha yao, unaowafanya kuwa kweli ni vyombo kwa waamini kuweza kumkimbilia
Mungu na Kristo wake. Mapadre wajitahidi kumtazama Kristo kama mfano na kielelezo
cha kuigwa. Watambue kwamba, Yesu ndiye mwalimu na mlezi mkuu wa Mapadre wanaoendeleza
huruma takatifu kati ya watu wake.