Serikali ya Tanzania yawatolea uvivu wanao dai hati ya Muungano!
Lifuatalo ni tamko la Katibu mkuu kiongozi kwa vyombo vya habari kuhusu hati ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar, iliyotolewa Ikulu, tarehe 14 Aprili 2014.
Siku 12
zijazo tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuzaliwa
kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wamezaliwa watu ndani ya Muungano huu na wengine
wana wajukuu. Inasikitisha sana kuwa leo, miaka 50 baadaye ipo dhana potofu inayojengwa
kuwa Muungano huu si halali kwa vile hakuna Hati ya Muungano (Articles of the Union).
Waasisi
wa Taifa letu ambao tarehe 22 Aprili, 1964 kule Zanzibar walitia saini Hati hiyo,
mbele ya mashuhuda, nao wameonekana kama walichokifanya kilikuwa kiini macho, na kwa
hiyo kwamba waliongoza Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msingi wa
kiini macho hicho kwa miaka yote hadi Mwenyezi Mungu alipowaita. Mambo yote mawili
yametusononesha sana sisi Serikalini, na bila shaka yamewasononesha wananchi wanaoipenda
nchi yao, wanaowapenda Waasisi wa Taifa letu na kuuenzi Muungano wao.
Madai
ya kuonyeshwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi lakini hatukuweza kuamini hali
itafikiwa ilipofikia, ambapo wapo watu wanathubutu kudai na kuapa kuwa Hati hiyo haipo.
Ukweli ni kuwa hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote. Hata hivyo, lazima tukubaliane
kuwa zipo Hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru
na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama mboni ya jicho. Hati hizo ni pamoja na
Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962,
na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964. Hati za aina hii zinahifadhiwa
maeneo maalum ambayo ni salama ili zisipotee wala kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi,
tunazifungua ili kuzihifadhi kwa namna yoyote ile.
Lakini sasa maneno yanakua
mengi, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi, kiasi cha wananchi kuanza
kutiwa mashaka iwapo kweli Hati ya Muungano ipo au la. Hivyo, kwa maagizo na ridhaa
ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ninaleta mbele yenu Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar
na waasisi wetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume, ili muione
na kuwahakikishia Watanzania kuwa yanayosemwa kuwa hakuna Hati hiyo si kweli. Hati
hiyo ipo tangu wakati huo, imetunzwa vizuri na waliotutangulia, tumeirithi, na tutaendelea
kuihifadhi. Na, tukiombwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge Maalum nina uhakika
Rais ataridhia ipelekwe huko ili kuondoa mjadala wa kama Hati ipo au la.
Isitoshe,
tufanye utaratibu wa kuweka nakala kwenye Makumbusho ya Taifa ili kila atakayetaka
kuiona katika miaka mingine 50 ijayo na kuzidi aione. Mwisho, narejea kusema kuwa
kwa upande wa Serikali tunasikitishwa na kufadhaishwa sana na tuhuma nzito kwamba
labda waasisi wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini macho. Hatukutarajia wawepo
Watanzania wenzetu, wafikie hapo.
Ni jambo zito. Vile vile hatukutarajia kuwa
Serikali itatuhumiwa kuwa haikuwa makini kuhifadhi waliosaini waasisi wetu. Matumaini
yetu ni kuwa baada ya leo tutaendelea na mambo ya msingi kwa mustakabali, umoja na
uimara wa Taifa letu badala ya kuchochea hisia kuwa Muungano wetu hauna msingi imara
wa kisheria.