Mchango wa waamini walei katika maandalizi ya mkutano mkuu wa AMECEA
Askofu mkuu Tarcisio Ziyaye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, hivi karibuni amezindua kamati ya waamini walei
75 kutoka Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi, kusaidia mchakato wa maandalizi ya maadhimisho
ya mkutano mkuu wa AMECEA unaotarajiwa kufanyika mjini Lilongwe, Malawi kuanzia tarehe
14 hadi tarehe 26 Julai 2014.
Kamati hii
inaundwa na wajumbe walioteuliwa kutoka katika Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la
Lilongwe kutokana na ujuzi, weledi na majitoleo yao katika maisha na utume wa Kanisa
nchini Malawi. Askofu mkuu Ziyaye amewashukuru na kuwapongeza waamini nchini Malawi
kwa kujitokeza kwa wingi pamoja na kuonesha nia ya kuchangia kwa hali na mali ili
kufanikisha maadhimisho ya mkutano wa AMECEA.
Kamati hii ya watu 75, itashirikiana
na Kamati nyingine ya watu 20 iliyokuwa imeundwa mwaka 2012 kwa ajili ya maandalizi
ya awali, hususan katika kutafuta fedha za kugharimia mkutano wa AMECEA. Kundi hili
kwa sasa limegawanyika katika kamati ndogo ndogo za: chakula, malazi, ulinzi na usalama,
matangazo, afya na protokali. Askofu mkuu Ziyaye amewataka waamini wanaotaka kutolea
muda wao kwa ajili ya kuwahudumia wajumbe wa mkutano wa AMECEA kujiandikisha mapema
Jimboni Lilongwe, kwani watu wengi zaidi watahitajika kwa ajili ya kutoa huduma.
Mkutano
mkuu wa AMECEA kwa Mwaka 2014 unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe 300 kutoka katika
nchi zinazounda AMECEA pamoja na wageni waalikwa. Hili ni tukio la Kikanisa litakalotoa
nafasi kwa Familia ya Mungu katika nchi za AMECEA kuweza kusali, kutafakari na kujadiliana
masuala yanayogusa maisha na utume wa Kanisa katika nchi hizi.