Mpendwa msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo.
Katika vipindi viwili vilivyopita, tulitafakari kwa uzito wa kutosha juu ya dhambi,
toba, msamaha na kujirekebisha. Leo tunahitimisha tafakari zetu zile mbili kwa kuzipa
muhutasari-unganifu.
Tunakubaliana
kimsingi kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa mwili, roho, akili na utashi. Katika makuzi
ya mtu, ni vema hayo yote manne yakue sambamba. Endapo mwili peke yake utakuwa huku
roho haikui, huyu mtu anakuwa mdumavu wa kiroho. Roho iliyodumaa ni hatari katika
maisha. Mtu mdumavu kiroho hana uhusiano mzuri na ulimwengu wa mambo ya kiroho, haoni
thamani ya Mungu katika maisha yake, haoni umuhimu wa sala na wala hafikiri maisha
baada ya halafu. Yeye maisha yake yote yamejaa sasa, basi. Na kwa upande mwingine,
endapo roho tu itakuwa na mwili utadumazwa, hiyo nayo ni hatari. Tushughulikie afya
ya roho na mwili, ili kuwa na makuzi sambamba.
Pamoja na hayo, sisi wanadamu
tumepewa akili na utashi. Kwa tafanusi nyepesi zinazosadifu tafakari yetu, tunaweza
kutafsiri akili kama uwezo wa kujua/kutambua/kupembua kati ya jema na baya. Akili
yetu inatusaidia kujua maana ya kitu au jambo na kupembua thamani yake huku tukihusisha
na maisha yetu na maisha ya wenzetu. Utashi ni uwezo wa ndani wa kuamua. Kile ambacho
akili inajua kuwa ni chema au kibaya, utashi sasa ndio hufanya kazi ya kuamua kutenda
au kutotenda.
Katika haya mawili pia, AKILI na UTASHI ni vema viwe na makuzi
sambamba. Tujibidishe kwa maumivu kabisa kukuza akili zetu kwa kujipatia maarifa mbalimbali
yaliyo mema yenye kutujenga. Tunafanya hivyo kwa kujisomea maandiko matakatifu, kuongea
na watu wenye hekima, kupata mafunzo mbalimbali ya maisha yetu nk. Tunaimarisha utashi
wetu kwa kujenga dhamiri iliyo njema, dhamiri yenye hofu ya Mungu, na kuimarisha ujasiri
ule wa kuamua kutenda au kutotenda lile ambalo akili yetu inalifahamu katika undani
wake.
Maarifa hayo mepesi yatusaidie kuelewa kwa nini sisi wanadamu tunakuwa
wepesi sana kurudi tena dhambini. Jibu hapo ni dhahiri, kwa wengine wetu ni kwa sababu
ya kwashakoo ya roho, au kwashakoo ya akili, au utapiamlo wa utashi au vyote kabisa.
Na tumeona jinsi ambavyo dhambi zinatutafuna na kutuangamiza katika maisha yetu ya
kila siku! Tunatubu, lakini dakika chache baadaye tunarudi kulekule. Ni kwa nini?
Tunajua tunachotenda? Lengo la kutubu lilikuwa ni nini? Tufanyeje ili walao tujitahidi
tusiporomokee tena madhambini? Kuna machache ya kuyazingatia hapa.
La kwanza,
tujue kwamba dhambi na maisha ya dhambi sio hulka ya mwanadamu. Mwanadamu ameumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu. Sehemu mmoja ya sura na mfano wa Mungu ni utakatifu wake.
Sisi wanadamu tunashiriki katika utakatifu wa Mungu. Dhambi ni doa linalokuja juu
ya utakatifu huo, hivyo huweza kuondoka na sisi tukabaki salama. Kwa neno hilo dogo,
tuelewe kwamba, sisi wanadamu tunaweza kujibidisha kuwa mbali na dhambi, tukaikimbia
na kuiacha kabisa.
Tatizo, wengi wetu tuna tabia ya kuikawaidisha dhambi.
Ukiizoe dhambi na dhambi ikakuzoea, unaingia katika mtego wa kujirafikisha na dhambi,
baadaye unaona ni kitu cha kawaida tu, na unaanza kufikiri na kujiaminisha kwamba
ni vigumu kuishi bila kutenda dhambi. Hapana, hapo tunajidanganya. Mwanadamu hana
undugu na dhambi, dhambi imekuja baadaye kama kupe na inaweza kuondoka na tukitaka
haiji tena.
Pili, tukumbuke daima UBAYA wa dhambi na matokeo yake. Dhambi haina
uzuri wowote, ni uangamizi tu, kama sio kwako mwenyewe basi kwa mwenzako, na kama
sio leo basi kesho. Tunaposema tusiitamadunishe dhambi, tunataka kwa akili safi kukataa
kabisa utamaduni wa dhambi, yaani kujiweka katika mazingira kwamba dhambi ni UTAMADUNI
WETU. Sasa kwa leo hii, kutokana na matumizi mabaya ya akili yetu na utashi wetu,
watu wengi tunatamadunisha dhambi, kwa kigezo cha haki za binadamu. Na hapo ndipo
wanapoingia katika msigano na Kanisa. Hatuwezi kabisa kuhalalisha mifumo ya dhambi
eti kwa kisingizio cha haki za binadamu.
Ni binadamu gani huyo mwenye HAKI
ya kuangamizwa na dhambi? Ni katika hayo sauti ya Kanisa kama mama na mwalimu kwa
watu wote na nyakati zote, itaendelea kusikika! Nani anaweza kuhalalisha mauaji ya
watoto kwa njia za uuaji mimba eti ni HAKI ZA BINADAMU? Ni nani mwenye akili safi
anayeruhusu kuchezacheza na sheria za kimungu mintarafu ndoa na familia, akalazimisha
miungano ya jinsia moja kwa kigezo cha haki za binadamu? Je, haki ya mtoto anayeasiliwa
na watu wa aina mmoja imezingatiwa? Ni nani mwenye haki ya kupanga haki ya mwenzake?
Ni katika mazingira hayo ndiyo tunajikuta katika utamadunishaji wa dhambi, kwa maangamizi
ya kizazi cha sasa na kijacho. Tunakwenda wapi?
Turudi kwenye misingi ya utu,
haki ya kweli na uhuru wa waana wa Mungu. Tunajikabidhi kwa shetani kwa kujua na kutaka
halafu tunadhani tutakuwa salama. Haiwezekani!! Kwa kila mtu binafsi, lazima kuwe
na ile nguvu ya kiutashi ya kujipatia katazo lenye nguvu, kusema HAPANA KAVU mbele
ya dhambi. Ni utashi wetu imara ndio utatusaidia tusiporomokee tena katika dhambi.
Tukiwa na utashi mtepetevu, daima tutajiangusha katika dhambi nyingi halafu
baadaye tunatafuta namna ya kuzihalalisha ili ziwe haki za binadamu. Sema hapana kwa
dhambi. Pamoja na hilo, lazima kuwa mwangalifu, usipende kujiweka katika mazingira
ya dhambi au kujiambatanisha na makundi ya kidhambi au asasi zenye milengo-shetani
ya waziwazi au iliyofichika.
Sisi kama jamii inayoishi sasa tunajiuliza swali
mmoja, huu uangamizi tunaoufanya saa, ungetendwa na wazee wetu tungejikuta katika
jamii ya aina gani duniani? Linaloonekana kwa nje ni kwamba jamii ya kimataifa haijibidishi
kabisa kumdhamirisha mwanadamu katika kutambua ubaya wa UOVU na matokeo yake, badala
yake inamhamasisha, inamlinda na kumsaidia mwanadamu kutenda madhambi zaidi, kwa kasi
zaidi na kwa uhuru zaidi (kwa kigezo cha haki za binadamu). HAPANA, hapo mama Kanisa
anasikitika, analia na kukataza kabisa. Tulinde, utu na uhuru wa kweli wa mwanadamu.
Sehemu
ya mwisho tuone, ni nani anawajibika kwa dhambi za jamii? Kama tulivyokwisha kutafakari
katika kipindi kilichopita juu ya aina ya dhambi, ni dhahiri kwamba kwa dhambi binafsi
ni mwanadamu kila mmoja kwa nafsi yake anawajibika mintarafu toba. Kwa dhambi za jamii
nani anawajibikia? Hapa tuseme tu kichungaji kwamba, ni mtu binafsi na jamii katika
umoja inawajibika. Kama ilivyo dhambi binafsi, huvuruga uhusiano wetu na Mungu, hali
kadhalika dhambi jamii huukorofi uhusiano wetu ndani ya jamii, tena huhaini uhusiano
wetu na vizazi vijavyo na juu zaidi huharibu uhusiano wetu na Mungu. Kumbe jamii lazima
ihusike.
Ni vema katika familia zetu katika mwaka, tuwe na siku mmoja ya kufanya
toba kwa dhambi za familia. Kutafakari, kufunga na kutubu yale yote ambayo tumeghafiriana
na kumkasirisha Bwana Mungu wetu. Pia katika jumuia ndogondogo, kigango, parokia,
jimbo hata taifa tufanye hivyo.
Katika uangamizi wa familia ya mwanadamu huenda
mimi na wewe tumeshiriki kwa namna fulani. Hatuwezi kunyamaza na kusema ‘ni hali ya
kawaida tu’. Dhambi siyo hali ya kawaida, NI HALI YA HATARI.Tuikimbie dhambi, nasi
tutakuwa salama. Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin
Mkorwe, OSB.