2014-04-13 14:48:01

Vijana kutoka Krakovia wakabidhiwa Msalaba wa Siku za Vijana Duniani


Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya Matawi, Baba Mtakatifu Francisko alitambua kwa namna ya pekee uwepo wa wajumbe mia mbili hamsini waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa kimataifa kuhusu Siku za Vijana Duniani, mkutano ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la Walei.

Huu ni mwanzo wa maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 itakayofanyika Jimbo kuu la Krakovia, Poland, kwa kuongoza na kauli mbiu "heri wenye rehema maana hao watapata rehema". Baba Mtakatifu amewakabidhi Msalaba wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, wajumbe kutoka Krakovia. Huu ni Msalaba wa Ukombozi ambayo Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, miaka thelathini iliyopita aliwakabidhi vijana na kuwataka kuutembeza sehemu mbali mbali za dunia kama alama ya upendo wa Yesu kwa binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 27 Aprili 2014, Mama Kanisa atakuwa na furaha ya pekee kabisa kwa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II, kuwa ni watakatifu. Mwenyeheri Yohane Paulo II ni muasisi wa Siku za Vijana Duniani atakayetangazwa na Mama Kanisa kuwa ni Msimamizi wa Siku za Vijana Duniani kwa kushirikiana na umati wa watakatifu ataendelea kuwa ni Baba na Rafiki kwa vijana wa kizazi kipya. Msalaba na Sanamu ya Bikira Maria Afya ya watu wa Roma ni kielelezo cha matumaini na upendo wa Kristo kwa walimwengu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu ametambua pia uwepo wa wajumbe kutoka Rio de Janeiro na Krakovia walioandamana na Maaskofu wao wakuu. Baba Mtakatifu anasema, panapo majaliwa, hapo tarehe 15 Agosti 2014, huko Daejeon, jamhuri ya Watu wa Korea, atakutana na vijana kutoka Barani Asia watakaokuwa wanaadhimisha Siku ya Sita ya Vijana wa Asia inayoongozwa na kauli mbiu "Ondoka, uangaze, kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia".

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wote kumwendea Bikira Maria, ili aweze kuwasaidia kumfuasa daima Kristo kwa imani na mapendo thabiti.







All the contents on this site are copyrighted ©.