2014-04-13 14:46:12

Kanisa linaingia kwenye Maadhimisho ya Juma kuu ili kuadhimisha Fumbo la Pasaka


Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, Kanisa linamshangilia Kristo alipoingia Yerusalemu kwa shangwe na watoto wa Wayahudi wakatandaza nguo zao njiani. Hii ni siku ya vijana kijimbo, inayoongozwa na kauli mbiu, "Heri maskini wa roho maana ufalme wa mbingu ni wao".

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kubariki matawi, umati wa vijana ulianza maandamano kuelekea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, huku wakiimba kwa shangwe. Baba Mtakatifu katika Ibada hii ametumia Fimbo ya Kiaskofu aliyozawadiwa na wafungwa kutoka gereza la Sanremo, Italia. Huu ni mwanzo wa maadhimisho ya juma kuu, Kanisa linapokumbuka mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anatawaka waamini kujitafakari kwa kuangalia hali yao mbele ya Yesu, kama wako kweli na hamasa ya kuonesha furaha na kumshangilia, au wamejikunyata na kumwangalia tu kama "nyanya mbichi". Katika shida na mahangaiko ya Yesu, waamini wanajisikia namna gani na wako upande gani? Je, ni kati ya kundi la wakuu wa Makuhani na Waandishi waliokuwa wanasubiri fursa ya kumkamata na kumsulubisha Yesu?

Je, wao pia ni sehemu ya akina Yuda Iskarioti waliomuuza Yesu kwa vipande thelathini vya fedha? Au ni kati ya Mitume waliokuwa wanauchapa usingizi wakati Yesu anakabiliana na mateso makali? Baba Mtakatifu anawauliza waamini ikiwa kama wanataka njia ya mkato kwa kutumia upanga kama ambavyo alitaka kufanya Mtakatifu Petro? au Yuda aliyemsaliti Yesu kwa busu la unafiki? Au Wazee wa Baraza wanaofanya kila mbinu kwa kutafuta mashahidi wa uwongo ili kumtia Yesu hatiani kwa kudhani kwamba ni kwa ajili ya mafao ya wengi?

Baba Mtakatifu anaendelea kuwauliza waamini ikiwa kama wanafanana na Pilato anapoona kwamba, "maji yamezidi unga" ana nawa mikono ili kukwepa wajibu wake kwa kuwashirikisha wengine. Katika hali ya kuchanganyikiwa na vurugu, Je, hata waamini nao wanaendelea kupiga kelele wakitaka Barabara afunguliwe na Yesu ahukumiwe kifo ili kuwafurisha watu na kumdhalilisha Yesu au kama wale Askari waliomdhihaki, wakampiga mijeledi na kumtemea mate usoni?

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake ambayo yalikuwa ni tafakari inayomshirikisha mwamini binafsi anawauliza ikiwa kama kweli wamekuwa na ujasiri wa Simoni wa Kirene aliyeshurutishwa kumsaidia Yesu kubeba Msalaba wake naye kwa upendo mkubwa akatekeleza dhamana hii! Kuna watu waliokuwa wanapita mbele ya Msalaba wakimdhihaki Yesu kwa vile alijiaminisha kuwa ni Mwana wa Mungu. Baba Mtakatifu anawauliza waamini, Je, hata wao wanajisikia kuwa na jeuri hata kumdhihaki na kumkejeri Mwana wa Mungu?

Bikira Maria na baadhi ya wanawake wajasiri, walisimama chini ya Msalaba kwa ujasiri mkubwa, wakateseka pamoja na Yesu katika hali ya ukimya!, Je, waamini nao wanaendelea kuteseka na Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku, tayari kama Yusufu wa Arimatayo kwenda kuchukua Mwili wa Yesu ili kuuzika au wanawake waliokuwa wanalia mbele ya kaburi la Yesu au wale Askari walioomba ulinzi mkali kwenye Kaburi la Yesu aliyekuwa ametangaza kwamba, baada ya Siku tatu angefufuka kutoka katika wafu? Hawa ni watu waliokuwa wanataka kuzuia maisha mapya kwa njia ya ufufuko wa Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ni maswali msingi ambayo yanaweza kuwasaidia waamini katika tafakari ya maadhimisho ya Juma kuu, Kanisa linapotafakari Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.