Yesu peke yake ndiye anayetoa maana ya kashfa ya mateso ya mtu mwadilifu!
Wajumbe wa kongamano la Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa ugonjwa wa Saratani nchini
Italia, lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha La Sapienza mjini Roma na Hospitali ya ya
Mtakatifu Andrea, Jumamosi, tarehe 12 Aprili 2014 walikutana na kuzungumza na Baba
Mtakatifu Francisko mjini Vatican ambaye amewapongeza kwa huduma makini katika kuwahudumia
wagonjwa.
Anasema, tafiti za kisayansi zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia,
kutibu pamoja na kugundua tiba ya magonjwa mbali mbali. Madaktari ni watu wanaotekeleza
dhamana kubwa na nyeti katika maisha ya watu, kwani wanapaswa kutoa majibu na matumaini
kwa wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, changamoto ya kumthamini mwanadamu
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; mwenye mwili na roho. Ugonjwa ni kielelezo
cha maumivu na mateso ya mtu mzima na wala si sehemu tu ya mwili wake.
Baba
Mtakatifu anasema kwa dhati kwamba, mwanadamu anahitaji kupata huduma makini ya tiba
pamoja na kuonja mshikamano wa kibinadamu, kisaikolojia, kijamii na maisha ya kiroho
pamoja na msaada kutoka kwa wanafamilia ya mgonjwa. Kutokana na ukweli huu, kuna haja
kwa wahudumu katika sekta ya afya kuwa na mwono mpana kuhusu mwanadamu na kutoa mwelekeo
wa kiutu kwa mgonjwa.
Baba Mtakatifu anawaalika kushirikiana kidugu na wagonjwa,
ili kuwasaidia kugundua uzuri wa maisha hata katika hali tete, ili kutambua na kuenzi
utu na heshima ya binadamu, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake
hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.
Baba Mtakatifu
anawatakia wajumbe wote kheri na baraka tele katika maadhimisho ya Juma kuu litakalokamilika
kwa mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Hapa Yesu aliweza kuumwilisha ubinadamu
na uliokombolewa na Mwenyezi Mungu, ambaye ni chemchemi ya upendo. Yesu peke yake
ndiye anayeweza kutoa maana ya kashfa ya mateso kwa mtu mwadilifu. Kristo aliyeteswa,
akafa na kufufuka awe ni dira ya utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Chini
ya Msalaba, waamini wanapata fursa ya kukutana na Yesu pamoja na Mama yake anayeteseka.
Huyu ni mama wa wote ambaye yuko daima karibu na watoto wake wagonjwa, akiwa na imani
thabiti pasi na kutetereka. Baba Mtakatifu anawaombea kwa Bikira Maria ili aweze kuwasaidia
katika tafiti na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.