2014-04-12 09:15:38

Jumuiya ya Kimataifa imeamua kujifunga kibwebwe kupambana na biashara haramu ya binadamu!


Mkutano wa pili katika harakati za kupambana na biashara haramu ya binadamu umehitimishwa hivi karibuni mjini Vatican kwa kuwashirikisha viongozi wa Kanisa, Wakuu wa Jeshi la Polisi pamoja na wadau mbali mbali katika vita dhidi ya biashara haramu ya binadamu.

Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu "Mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu: Kanisa na utekelezaji wa sheria. Lengo la mkutano huu lilikuwa ni kuibua mbinu mkakati wa kupambana na biashara haramu ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia kwa kushirikiana na vyombo vya sheria. Baba Mtakatifu Francisko ameridhia mkutano huu na kuzungumza pamoja na wajumbe waliohudhuria mkutano huu kwa kuwataka kuchukua hatua madhubuti katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, kwani hivi ni vitendo vinavyo dhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Katika tamko lao, wajumbe wa mkutano huu wanasema, kama watekelezaji wa sheria katika Jumuiya ya Kimataifa wanapenda kujitosa kupambana na hatimaye kuling'oa kabisa janga hili ambalo ni mwendelezo wa vitendo vya jinai dhidi ya wanyonge ndani ya Jamii. Mkutano huu ni sehemu ya mchakato wa ushirikiano katika ngazi ya kimataifa, ili kuibua mbinu mkakati wa kuzia, kuwahudumia na kuwashirikisha waathirika katika maisha ya Kijamii, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa waathirika.

Viongozi hao wanasema, kwamba, wataendelea kushirikiana na Kanisa, vyama vya kiraia pamoja na wadau mbali mbali ili kuwafikisha kwenye mkondo wa sheria wahusika wa biashara haramu ya binadamu inayoendelea kusababisha mateso makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia.







All the contents on this site are copyrighted ©.