Tume ya Kipapa ya Sayansi za kihistoria, Mwaka huu inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka
sitini tangu ilipoanzishwa na Papa Pio wa kumi na mbili na wakati wote huu, imelihudumia
Kanisa kwa weledi na tija, kiasi cha kuliwezesha Kanisa kuwahamasisha walimwengu kutafuta
ukweli unaojikita katika undani wa moyo wa wanadamu!
Baba Mtakatifu Francisko,
akizungumza na wajumbe wa tume hii, Jumamosi, tarehe 12 Aprili 2014 amewakumbusha
kwamba, katika tafiti na mafundisho yao wanakutana na Kanisa linalosafiri katika nyakati
na historia yake ya Uinjilishaji, matumaini na mapambano ya kila siku; haya ni maisha
ambayo yanajikita kwa namna ya pekee katika huduma ambayo si haba. Lakini kwa upande
mwingine, wanaona ukosefu wa uaminifu, hali ya kukata tamaa na uwepo wa dhambi.
Baba
Mtakatifu anawaambia kwamba, tafiti zao zikiwa zimesheheni upendo kwa Mama Kanisa
na ukweli, zinaweza kuwa ni msaada mkubwa katika kung'amua kile ambacho Roho Mtakatifu
anapenda kuliambia Kanisa kwa sasa. Tume hii ni sehemu ya ushirikiano na taasisi mbali
mbali duniani, inayowasindikiza wasomi katika tafiti zao, kama sehemu ya mchango wa
Kanisa katika kukuza na kuendeleza majadiliano na ulimwengu mamboleo.
Baba
Mtakatifu Francisko anawaalika kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Karne moja,
tangu vita kuu ya kwanza ya dunia ilipofumuka na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa
watu na mali. Ni vyema, wakaangalia kwa umakini mkubwa mchango wa Vatican katika masuala
ya kidiplomasia, msaada uliotolewa na Wakristo katika kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi,
wahamiaji na majeruhi wa vita; watoto yatima, wajane.
Papa Benedikto wa kumi
na tano akizungumzia kuhusu vita hii aliwahi kusema kwamba, ni janga lisilokuwa
na mashiko! Hata leo hii bado Mama Kanisa anaendelea kuhimiza kwamba, kwa njia ya
amani hakuna kinachoweza kutoweka, lakini kwa vita kila kitu kinapotea. Maneno haya
ya kinabii yaisaidie Jumuiya ya Kimataifa kutambua kwamba, historia ni mwalimu wa
maisha.