2014-04-11 16:20:49

Uelewa wa kiroho kuhusu Maandiko Matakatifu


Baba Mtakatifu Francisko, wasaidizi wake wa karibu pamoja na viongozi mbali mbali wa Kanisa, Ijumaa tarehe 11 Aprili 2014 wameshiriki katika tafakari ya tano iliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya kipapa wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima. Amekazia umuhimu wa uelewa wa maisha ya kiroho kuhusu Maandiko Matakatifu mintarafu mafundisho ya Mtakatifu Gregori mkuu.

Padre Cantalamessa anasema, kuna haja ya kupyaisha na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha ya kila siku, kwani Neno la Mungu ni nguzo ya maisha. Bado Mama Kanisa anapenda kuongozwa na dira iliyotolewa na Mababa wa Kanisa wakati wa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu.

Waamini wanapaswa kutambua ukuu wa Yesu Kristo kama nguzo ya imani yao, umuhimu wa Neno la Mungu kwa kuzingatia Mafundisho na Mang'amuzi ya Kanisa kuhusu Maandiko Matakatifu, kama Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanavyofundisha katika Waraka wake wa Neno la Mungu, Dei Verbum. Biblia ni maneno ya Mungu yaliyotamkwa kwa lugha lugha za kibinadamu yameingia katika maneno ya wanadamu, kama ambavyo Mababa wa Mtaguso wa Nicea wa Mwaka 325 wanavyokiri na kufundisha juu ya Umungu wa Kristo.

Yesu ni utimilifu wa unabii na sheria katika Agano la Kale kwa kumwilisha maneno na matendo yake, anafungua ukurasa wa Agano Jipya unaojikita katika majadiliano na ujenzi wa Jumuiya ya Wakristo wanaoshuhudia ukuu wa Yesu katika ulimwengu huu. Mababa wa Kanisa wameonesha kwamba, Maandiko Matakatifu ni nguzo na dira ya maisha ya waamini.Biblia inaweza kuelezwa katika nyanja kuu tatu: Kisarufi na kihistoria; kwa njia ya mifano rejea katika imani kwa Kristo; kimaadili kama kanuni inayoongoza maisha ya Mkristo na kuhusu mambo ya nyakati.

Padre Cantalamessa anasema, Kanisa bado linahitaji kuongozwa na tafakari ya Mababa wa Kanisa katika tafakari ya Neno la Mungu, ili kugundua umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya kiroho kwa kukazia Mafundisho ya Mababa wa Kanisa kuhusu Biblia: kihistoria, kimafumbo, kimaadili na kwa ajili ya mambo ya nyakati. Kweli zilizofunuliwa na Mungu zilizomo na zinazoelezwa katika Maandiko Matakatifu, zimeandikwa chini ya uvuvio wa Roho Mtakatifu.

Imani thabiti juu ya Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha ya Mkristo na kwamba ni nyenzo makini katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya na utamadunisho, ili kwamba, Neno la Mungu liweze kusafisha tamaduni za watu kwa njia ya kweli za Kiinjili. Lakini, kwanza kabisa Neno la Mungu linapaswa kumwilishwa na watangazaji kwa njia ya ushuhuda amini na makini wa maisha, ili kuwaonjesha wengine furaha ya Neno la Mungu. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika maisha ya Wakristo. Wakristo wakumbuke kwamba, katika maisha yao wamepewa zawadi ya Kristo na Biblia.







All the contents on this site are copyrighted ©.