Simameni kidete kupambana na utumwa mamboleo unaowanyanyasa watoto!
Chama cha Kimataifa cha Kutetea Watoto, BICE, kilianzishwa na kuridhiwa na Papa Pio
wa kumi na mbili mara tu baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia, ili kulinda na kuwatetea
watoto, harakati zilizochangia hata kuanzishwa kwa itifaki ya Umoja wa Mataifa kwa
ajili ya watoto kunako mwaka 1989. BICE inaendeleza ushirikiano na Ubalozi wa Vatican
kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa.
Changamoto kubwa kwa sasa ni kusimama kidete
kupambana na utumwa mamboleo unaowafanyisha watoto kazi za suluba, kuwanyanyasa pamoja
na kuwadhulumu. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watoto wanapata haki ya kuishi na
kukua katika familia, wakiwa na wazazi wao wawili, yaani Baba na Mama, ili kuweza
kufikia ukomavu katika mahusiano. Wazazi pia wanachangamotishwa kutekeleza wajibu
wa kuwapatia watoto elimu inayojikita katika maadili, utu wema na maisha ya kiroho.
Ni
changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza
na wajumbe wa Chama cha Kimataifa cha kutetea watoto, waliomtembelea mjini Vatican,
Ijumaa tarehe 11 Aprili 2014. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ikiwa kama
watu wataendelea "kuchakachua" mifumo ya elimu, kuna hatari ya kukumbana na maafa
kama ilivyojitokeza katika karne iliyopita kwa kuwasukumiza watoto na vijana kutembea
katika "mawazo mgando".
Baba Mtakatifu anasema, kutetea haki msingi za binadamu
kunahitaji majiundo makini ya kiutu kwa kumtambua binadamu na utu wake; kwa kujibu
kikamilifu shida na changamoto anazokumbana nazo katika tamaduni mamboleo zinazoenezwa
kwa kiasi kikubwa na vyombo vya upashanaji habari. Chama cha BICE hakina budi kujikita
katika majiundo makini ya wanachama na wafanyakazi wake kuhusu utu na heshima ya watoto,
kwani hapa ni kiini cha haki zao msingi na mipango yote ya elimu na malezi.