2014-04-11 11:23:00

Pambaneni na vishawishi kwa kukumbatia utakatifu na maisha adili!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Ijumaa tarehe 11 Aprili 2014 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican anasema kwamba, Yesu katika maisha na utume wake, alipambana kufa na kupona na vishawishi pamoja na nguvu za Shetani, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kupambana na dhambi, kwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha.

Wafuasi wa Kristo wanapaswa kutambua kwamba, Yesu alijaribiwa, akadhulumiwa na hatimaye akauwawa Msalabani, mwaliko kwa waamini kumtolea Kristo ushuhuda wa maisha adili na utakatifu unaojikita katika maisha ya Jumuiya ya waamini. Vishawishi vya Yesu vilifafanuliwa kwa kina na mapana mwanzoni mwa Kipindi cha Kwaresima.

Vishawishi hivi vimejionesha pia kwa Adamu na Eva. Vishawishi dhidi ya Yesu vimeendelea kukua na kupanuka, kiasi hata cha kugusa Nafsi yake kama Mwana mpendwa wa Mungu, wengi wakajikwaa na kuanguka, wakatka kumfutilia mbali kutoka katika uso wa dunia. Katika mapambano haya, kuna watu wengi walioguswa na ushuhuda wa maisha na matendo yake, kiasi cha kumtolea Mungu utukufu na sifa. Walimtambua kwamba ndiye Kristo na Masiha wa Bwana, aliyetumwa kuja duniani kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na kifo kwa njia ya Fumbo la Msalaba.

Baba Mtakatifu anawahimiza Wakristo na watu wenye mapenzi mema kupambana kufa na kupona dhidi ya Shetani, dhambi na vishawishi, kwa kukumbatia utakatifu na maisha adili, kielelezo makini cha mfuasi wa Yesu Kristo. Baba Mtakatifu anakazia kwamba, Shetani yupo na wala si nadharia, ukicheza utabwaga chini na hapo ndipo utakapotambua makali yake! Neno la Mungu liwajengee waamini uwezo wa kupambana na vishawishi pamoja na uwepo wa dhambi!







All the contents on this site are copyrighted ©.