Mwenyeheri Yohane Paulo II mtetezi wa haki na amani
Haki na amani ni kati ya maneno makuu yaliyotumiwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II katika
maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni kiongozi aliyetoa hamasa
kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kupenda na kudumisha misingi ya haki na amani kwani
amani ni tunda la haki na mapendo.
Amani ina
msingi wake katika uelewa sahihi wa binadamu unaojikita katika katika haki na mapendo.
Watu wanapaswa kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani kwa njia ya majadiliano
ya kina kama suluhu ya migogoro na kinzani zinazojitokeza katika maisha ya mwanadamu,
kwani kushindwa kwa misingi ya amani matokeo ya vita!
Hivi ndivyo Kardinali
Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki
anavyomkumbuka Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, kama sehemu ya Katekesi endelevu za
Kipindi cha Kwaresima na kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya kumtangaza
kuwa Mtakatifu. Tafakari hii imetolewa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Giusto Jimbo
Katoliki Trieste, Italia.
Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipenda kujikita
katika amani kwa njia ya majadiliano ya kidini na kiekumene, mambo ambayo yalikuwa
yanabubujika kutoka katika undani wa tasaufi yake; iliyounganisha mawazo na matendo
yaliyomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu. Kwa njia hii, Mwenyeheri Yohane
Paulo II alifanikiwa kuleta mageuzi makubwa duniani na kwa namna ya pekee Barani Ulaya.
Kuta za chuki na uhasama wa kisiasa zikamobolewa, wananchi wakapata uhuru wa kujenga
na kudumisha mshikamano wa upendo na kidugu.
Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili
aliyeonja suluba na mateso ya vita kuu ya pili ya dunia, aliweka dhana ya amani kuwa
ni kati ya mafundisho yake makuu, kwa waamini na wale wasioamini, kwani vita inapofumuka
haina pazia wala macho! Kwa mwamini, amani ni kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo
na kwamba, hii ni zawadi ambayo Kristo amewaachia wafuasi wake, hivyo wanayo dhamana
ya kulinda, kuitetea na kuiendeleza, kwa kuanzia kwa wao wenyewe ambao wanapaswa kuwa
kweli ni vyombo vya amani.
Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili anasema Kardinali
Sandri kwamba, hakusita kuwakemea viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waliokuwa wanatumia
vita kama njia ya kufikia suluhu na maamuzi yao ya kisiasa. Kardinali Sandri anasema,
kamwe hatasahau pale aliposimama kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican kuitangazia dunia kwamba, Papa Yohane Paulo II amefariki dunia. Moyo wake
ulishikwa na simanzi na huzuni kubwa sana!