Yohane XXIII na Yohane Paulo II ni miamba wa imani na utakatifu wa maisha!
Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma katika Barua yake kwa
waamini wa Jimbo kuu la Roma anasema kwamba, tukio la Mama Kanisa kuwatangaza Wenyeheri
Yohane wa XXIII pamoja na Yohane Paulo II kuwa watakatifu hapo tarehe 27 Aprili 2014
ni tukio la neema na baraka kwa Kanisa zima, linalopokelewa na Jimbo kuu la Roma kwa
mikono miwili. Hawa ni miamba wawili walioasisi na kumwilisha Mafundisho ya Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Ni Maaskofu
waliotekeleza utume na maisha yao hapa Roma kama Makhalifa wa Mtakatifu Petro; wakawa
ni waalimu wa imani, maadili na utu wema kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Ni viongozi
waliojitosa kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, wakitoa
kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii
kutokana na hali n anafasi zao katika Jamii iliyokuwa inawazunguka.
Viongozi
hawa wawili, walikazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa adhimisho la Fumbo la
Ekaristi Takatifu kama kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, kwa kutoa mwaliko
kwa waamini kushiriki kikamiluifu katika Ibada ya Misa Takatifu. Hii ilikuwa ni njia
muafaka ya kujenga na kudumisha uhusiano kati ya mwamini na Yesu Kristo unaopaswa
pia kuendelezwa kwa njia ya sala na maisha adili.
Mwenyeheri Yohane XXIII kwa
ushupavu na imani thabiti, alithubutu kufungua ukurasa mpya wa maisha na utume wa
Kanisa kwa kuitisha Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ambao Kanisa linaendelea kushuhudia
matunda yake, kwa kusoma alama za nyakati. Yohane Paulo II katika maisha na utume
wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, alijitahidi kumwilisha Mafundisho ya Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kufanya
rejea katika Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na hatimaye,
kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao.
Kardinali Agostino
Vallini anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutumia kipindi hiki cha
Kwaresima kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya kushiriki kikamilifu katika mchakato
wa Mama Kanisa wa kuwatangaza Wenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II kuwa ni
watakatifu, hapo tatehe 27 Aprili 2014, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro utakapofurika
kwa umati mkubwa wa waamini na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia.