2014-04-10 07:24:14

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Vijana Kijimbo kwa Mwaka 2014


Jumapili ya Matawi, Kanisa linaadhimisha Siku ya Vijana Duniani katika ngazi ya Kijimbo, inayoongozwa na kauli mbiu “Heri maskini wa roho, maana ufalme wa mbingu ni wao”. (Mt. 5:3). RealAudioMP3

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 29 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2014, bado anakumbuka maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Hili lilikuwa ni tukio la imani na udugu, lililopambwa na kupambika kwa wema pamoja na ukarimu wa wananchi wa Brazil ulioshuhudia umati mkubwa wa vijana ukifurika katika ufuko wa Copacabana, changamoto kwa kila mwamini kuendelea kuwa ni mfuasi wa Yesu na Mmissionari, ili kuweza kuwashirikisha wengine hazina hii muhimu katika maisha.

Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 itaadhimishwa Jimbo kuu la Krakovia, nchini Poland. Katika kipindi cha miaka mitatu, vijana wataendelea kutafakari juu ya Heri za Mlimani. Mwaka huu, vijana wanatafakari kuhusu Heri ya kwanza, yaani “Heri maskini wa roho, maana ufalme wa mbingu ni wao”. Kwa mwaka 2015 vijana wanaalikwa kutafakari kuhusu “Heri wenye usafi wa moyo, maana ufalme wa mbingu ni wao” na kwa Mwaka 2016 kauli mbiu ni “Heri wenye huruma, maana hao watahurumiwa”.

Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha vijana kufanya tafakari ya Heri za Mlimani kwani haya ni Mafundisho Makuu ya Yesu aliyoyatoa pale kando la Ziwa la Galilaya. Mlimani kadiri ya Maandiko Matakatifu ni mahali pa ufunuo ambako Mwenyezi Mungu anapenda kukutana na watu wake. Yesu anatumia fursa hii ili kuwashirikisha wafuasi wake chemchemi ya maisha, kwa kujifunua kama Mwalimu na Musa mpya.

Yesu anajionesha kuwa ni njia inayobubujika furaha tangu pale alipozaliwa hadi alipokufa juu ya Msalaba na hatimaye, kufufuka siku ya tatu, matukio yote haya yanaonesha jinsi ambavyo alimwilisha Heri za Mlimani katika maisha yake na kukamilisha ahadi za Ufalme wa Mungu. Yesu anawaalika wafuasi wake kutembea pamoja na ye katika njia ya upendo inayowapeleka katika uzima wa milele. Hii njia inayosheheni magumu, lakini Yesu ameahidi kwamba, ataendelea kuwa pamoja nao hadi utimiifu wa dahali. Watakumbana na umaskini, watateswa na kunyanyaswa, watapamba na na ukosefu wa haki na changamoto za toba ya wongofu wa ndani, bila kusahau mapambano yanayowataka kuchuchumilia utakatifu wa maisha.

Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu, watakabiliana na changamoto mbali mbali za maisha, mwaliko wa kuendelea kushirikiana na Yesu katika furaha na mateso, katika magumu na hali ya kukata tamaa. Kwa kushikamana na Yesu anasema Baba Mtakatifu, waamini wataweza kupata amani na furaha inayobubujika kutoka kwenye upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Heri za Mlimani ni nguvu ya mabadiliko mapya inayoleta mageuzi ya furaha ya kweli na wala si kama ile inayotolewa na vyombo vya upashanaji habari. Inashangaza masikioni mwetu kwamba, Mwenyezi Mungu amejitwalia ubinadamu, akawa sawa na binadamu, hata kufa Msalabani.

Kwa mantiki ya ulimwengu huu, wale ambao wanahesabiwa na Yesu kuwa wana heri, ni watu wanyonge na waliopoteza dira na mwelekeo! Wanatukuzwa wale wanaoonesha mafanikio, wenye mamlaka, nguvu na wenye kuheshimiwa na watu! Hii ni changamoto kubwa ya imani, inayowaalika vijana kuchukua Msalaba wao na kuanza safari ya kumfuasa Yesu, kwani Yeye anayo maneno ya uzima. Vijana wakithubutu kumkubali na kumpokea Yesu katika maisha yao ya ujana, atawajaza furaha na maana halisi ya maisha!

Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kuwa ni watu wenye furaha inayosimikwa katika imani na ukweli, mambo yatakayowawezesha kuwa na mang’amuzi ya kweli katika maisha kwa kukataa njia za mkato ambazo mara nyingi zinahatarisha maisha yao kwa kuwatumbukiza katika raha, starehe na anasa, mambo ambayo kamwe hayawezi kuzima kiu ya maisha yao ya ndani. Inasikitisha kumwona kijana akiogelea katika utupu!

Vijana wanapaswa kuwa imara wakiwa wanaongozwa na Neno la Mungu katika maisha yao, tayari kushindana na malimwengu, wakiwa na ujasiri unaowaongoza kutafuta furaha ya kweli pamoja na kuzingatia mambo msingi katika maisha. Kwa njia hii vijana wataweza kuwajibika na kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri mkuu.

Baba Mtakatifu anasema, umaskini wa roho unajionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, pale Yesu alipojitwalia hali ya binadamu akawa sawa na binadamu na wala hakuona kwamba, kuwa sawa na Mungu ni jambo la kung’ang’ania sana. Hapa Mwenyezi Mungu anaamua kuukumbatia umaskini, ili aweze kumtajirisha mwanadamu kwa umaskini wake. Hili ndilo Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, kwa kuonesha unyenyekevu na upendo wa hali ya juu kabisa kwa mwanadamu. Mtakatifu Francisko wa Assisi ni kielelezo na mfano wa kuigwa katika umaskini wa roho, kwa kuonesha upendo kwa Kristo, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Umaskini wa roho ni changamoto na mwaliko wa kubadilisha mfumo wa maisha kwa kuwa huru na vitu wala kutokubali kumezwa na malimwengu: utajiri na mali na matokeo yake mambo haya yanawaachia machungu katika maisha. Vijana wanahamasishwa kujiaminisha mbele ya Mungu anayewapenda na kamwe hatawasahau, jambo la msingi ni kuwa na ujasiri wa furaha na kiasi. Vijana wanaalikwa na Mama Kanisa kwa namna ya pekee kutubu na kuongoka, kwa kukazia upendo na mshikamano wa kidugu katika mchakato wa kukabiliana na hali ya umaskini unaojionesha katika: ukosefu wa fursa za ajira, wahamiaji, matumizi haram ya dawa za kulevya na utumwa mamboleo. Vijana wawe ni kikolezo cha: ujasiri, upendo na matumaini mapya miongoni mwa vijana wenzao. Maskini ni fursa ya kukutana na Yesu mteseka!

Baba Mtakatifu anasema hata maskini katika umaskini wao, wanayo mengi ya kuwashirikisha na kuwafundisha. Hawa ni kama Mtakatifu Benedikto Giuseppe Labre aliyekuwa analala kwenye mitaa ya mji wa Roma, lakini alibahatika kuwa ni mshauri mkuu wa maisha ya kiroho hata kwa watu mashuhuri kwenye Karne ya kumi na nane. Utu wa mtu una thamani kubwa na wala si kiasi cha fedha alicho nacho kwenye akaunti yake Benki. Maskini ni walimu wa unyenyekevu na matumaini kwa Mungu, wanaotambua udhaifu wao, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Yes uni kiini cha Habari Njema ya Wokovu na ujenzi wa Ufalme wa Mungu ambao Mama Kanisa anasali daima ili uweze kuwafikia watu wengi zaidi, kwa kuhakikisha kwamba, Wakristo wanajitokeza kifua mbele kwenda kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kanisa halina budi kukumbatia Ufukara wa Kiinjili ili kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu. Uinjilishaji Mpya unawezekana tu, ikiwa kama utakuwa unabubujika kutoka katika Injili ya Furaha. Waamini wajenge na kuimarisha uhusiano na Mungu pamoja na jirani zao.

Kutangazwa kwa Wenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II kuwa Watakatifu liwe ni tukio linaloshehenesha furaha ya kweli miongoni mwa wafuasi wa Kristo na watu wote wenye mapenzi mema. Yohane Paulo II atakuwa ni mtakatifu msimamizi wa Siku za Vijana Duniani, kwani Yeye ni muasisi na mtekelezaji mkuu wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Kwa vijana wengi ataendelea kuwa ni Baba na Rafiki.

Kanisa pia linafanya kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu Vijana walipokabidhiwa Msalaba wa Ukombozi, ambao umetembelea sehemu mbali mbali za dunia. Kunako Mwaka 1984, Mwenyeheri Yohane Paulo II aliwataka vijana kuutembeza Msalaba wa Jubilee kuu ya Mwaka wa Ukombozi, kama kielelezo cha upendo wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Vijana Kijimbo kwa kusema kwamba, utenzi wa Bikira Maria, yaani “Magnificat” ni kielelezo cha mwanamke aliyejitahidi kumwilisha Heri za Mlimani. Injili ya Furaha inabubujika kutoka katika moyo wa Bikira Maria, ambaye vizazi vyote watamwita Mwenyeheri. Bikira Maria nyota ya Uinjilishaji Mpya awasaidie waamini kumwilisha Injili na Heri za Mlimani katika maisha kwa kuwa na ujasiri wa furaha.

Ujumbe huu umehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.