Onesheni thamani kwa Mji wa Roma, boresheni maisha kwa masomo na tunu bora za maisha
ya kiroho!
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 10 Aprili 2014 amekutana na kuzungumza na
Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriani, Taasisi ya Maandiko Matakatifu na
Taasisi ya Kanisa la Mashariki. Baba Mtakatifu anasema hizi ni taasisi ambazo ziliunganishwa
na Papa Pio kumi na moja kunako mwaka 1928 na kukabidhiwa chini ya usimamizi wa Shirika
la Wayesuit, kwa ajili ya kumtumikia Kristo, Kanisa na kuendelea kuwa waaminifu kwa
Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa ushirikiano
kwa kuendeleza kumbu kumbu za kihistoria ili kuziendeleza kwa siku za usoni kwa kuzingatia
kipaji cha ugunduzi, kinachowawezesha kupata mwelekeo mpana zaidi wa hali na changamoto
mamboleo ili kushirikishana na kuzipatia ufumbuzi kwa kutumia njia bora zaidi.
Baba
Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriani na taasisi zake
kuhakikisha kwamba, inathamini eneo wanalofanyia kazi na kusomea, yaani Jimbo kuu
la Roma. Hapa ni kuna mizizi ya imani, kumbu kumbu hai ya Mitume na Wafiadini; ni
mahali panapoonesha ukarimu, umoja na Ukatoliki. Hizi ni tunu zinazopaswa kuheshimiwa
na kuthaminiwa na wote.
Roma ni mji ambao unakusanya waamini kutoka katika
Makanisa mahalia, wanaokuja wakiwa na tamaduni na mapokeo yao; utajiri mkubwa kwa
vyuo vikuu vya kipapa pamoja na taasisi zake, changamoto ya kukuza na kuimarisha imani,
kwa kufungua akili na mioyo ili kuona Ukatoliki. Ni mwaliko wa kutoka pembezoni mwa
jamii na kuingia mjini kati, tayari kurudi tena pembezoni mwa Jamii kwa ajili ya kuhudumia.
Baba
Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na uwiano bora zaidi
kati ya masomo na maisha ya kiroho, kwa kurutubisha mahusiano haya kwa kuonesha upendo
thabiti kwa Yesu Kristo na Kanisa lake; kwa kujikita katika tafiti moyo inayogusa
ukweli na imani; mambo yanayofafanuliwa kwa kina na mapana katika masomo ya Falsafa
na Taalimungu yanayojikita katika sala, kwa kujinyenyekeza mbele ya Mwenyezi Mungu,
ili kutafuta ukweli ili kuuendeleza: kuuimarisha kadiri muda unavyozidi kusonga mbele.
Mwanataalimungu asiyesali wala kumwabudu Mwenyezi Mungu anaweza kuishia katika utupu!
Baba
Mtakatifu anasema, tafiti na masomo ni mambo ambayo hayana budi kumwilishwa katika
maisha ya mtu binafsi na jumuiya; katika dhamana ya kimissionari na udugu unaowashirikisha
hata maskini pamoja na kuhangaikia maisha ya ndani ili kujenga na kuimarisha uhusiano
na Yesu. Vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu ni Jumuiya zinazowasaidia wanafunzi
kukua na kukomaa kama ilivyo kwenye familia.
Viongozi wa Vyuo vikuu na taasisi
za elimu ya juu ni wakuu wa Jumuiya, changamoto ya kuonesha ari na moyo wa huduma
ili kujenga na kuimarisha tunu msingi za kifamilia katika uhalisia wa maisha ya kila
siku unaojikita katika ubinadamu na hekima, ili kuwajengea wanafunzi wanaohitimu masomo
yao, kuweza kutangaza kweli mintarafu ubinadamu. Bila kuthamini wema na uzuri wa familia,
kazi itageuka kuwa ni shughuli ya akili isiyokuwa na mashiko; mshika maadili pasi
na wema; mtaalam pasi na elimu wala uzuri, mtu anayeendeshwa na taratibu za kila siku.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema kwamba, mwingiliano wa kila siku unaojikita katika kazi
na ushuhuda unaotolewa na wafanyakazi wanaotekeleza dhamana yao kwenye Chuo kikuu
na Taasisi mbali mbali, watawaonjesha ukweli utakaosaidia sayansi wanazojifunza kuwa
kweli ni sayansi za kiutu na wala si maabara tu ya kuunda wasomi.
Baba Mtakatifu
anaitakia kheri na baraka tele Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriani pamoja
na taasisi zake kwa kuwaweka chini ya maombezi ya Bikira Maria kikao cha hekima na
ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola pamoja na watakatifu somo na wasimamizi wao.