2014-04-10 12:01:09

Msibinafsishe mawazo ya watu ni hatari kwa uhuru!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Siku ya Alhamisi, tarehe 10 Aprili 2014 anasema kwamba, hata leo hii kuna watu ambao wanataka kuhodhi mawazo ya wengine, jambo ambalo ni hatari sana kwa uhuru wa wananchi sanjari na uhuru wa kidhamiri, changamoto kwa waamini kukesha na kusali.

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu aliahidi kwamba, Ibrahimu atakuwa ni Baba wa Taifa kubwa ikiwa kama yeye na kizazi chake watakuwa waaminifu kwa Agano ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amefunga pamoja naye. Baba Mtakatifu anasema, watu wa Agano la Kale waling'oa kutoka mioyoni mwao Amri za Mungu, kiasi kwamba, zikakosa mwelekeo na mashiko katika maisha yao.

Yesu katika Agano Jipya na la Milele anaonesha mwelekeo mpya baada ya kukutana naye, lakini Mafarisayo bado wanaonesha shingo ngumu hawataki kuona mabadiliko, wanafung akili na mioyo yao dhidi ya Yesu, kiasi kwamba, hata Mwenyezi Mungu hana nafasi tena katika maisha yao. Wamekengeuka na kusahau maagizo waliyokuwa wamepewa na Mwenyezi Mungu, wakashindwa kuwa waaminifu kwa Manabii na Mwenyezi Mungu. Ni viongozi waliowatwisha watu mizigo mikubwa lakini wao wenyewe hawakuthubutu kuigusa hata kwa kidole chao!

Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kujenga na kukuza utamaduni wa kufanya majadiliano na Mwenyezi Mungu, kwa kuruhusu watu wengine pia kushirikisha mawazo yao, ili kusitokee tena na Madikiteta kama ilivyojitokeza kwenye Karne ya ishirini kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia, kwa vile tu kuna watu waliokuwa wanawapinga.

Kuna baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ili kuweza kutoa misaada wanalazimisha mawazo yao kama sehemu ya masharti ya kupewa msaada. Mwelekeo wa namna hii ni kudhalilisha uhuru wa watu sanjari na uhuru wa kujieleza bila kusahau uhuru wa kidhamiri.

Baba Mtakatifu anasema, hapa kuna haja ya kukesha na kusali bila kukoma, ili kweli watu waweze kupata uhuru ndani ya mioyo yao, ili kupokea na kumwilisha Neno la Mungu kama dira na mwongozo wa maisha yanayobubujikia katika furaha na Agano linalopaswa kuendelezwa mbele!







All the contents on this site are copyrighted ©.