2014-04-10 08:20:36

Imani, tamaduni na mafao ya wengi changamoto ya majadiliano ya kidini na wasioamini!


Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema kwamba, Kanisa linaendelea kufanya mchakato wa majadiliano ya kidini na wale wasioamini nchini Marekani mintarafu changamoto na mielekeo ya tamaduni katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 11 Aprili, mjini Washington DC, Marekani, Baraza la Kipapa limekuwa likiendesha mikutano mbali mbali ya majadiliano ya kidini na watu wasioamini.

Kauli mbiu inayoongoza mikutano hii ni "Imani, utamaduni na mafao ya wengi". Hapa majadiliano yamelenga kwa namna ya pekee kuangalia uhusiano kati ya Jamii na Serikali; uzoefu na mang'amuzi ya maisha ya kidini, ingawa Serikali inaendelea kuwa na malengo pamoja na utambulisho wake.

Kardinali Ravasi anasema, nchini Marekani, viongozi wa kisiasa wanaangalia kwa namna ya pekee mahusiano yao na mambo ya kidini, ingawa pia kuna mambo kadhaa ambayo wanasiasa nchini Marekani wanasigana kwa kiasi kikubwa na tunu msingi za maisha ya kidini. Viongozi kadhaa wa kidini wamechangia kuhusu umuhimu wa maisha ya kiroho katika maboresho ya demokrasia, ushirikiano kati ya viongozi wa kisiasa na vyombo vya upashanaji habari, kwa ajili ya kutafuta na kudumisha mafao ya wengi.

Kardinali Ravasi anabainisha kwamba, kunako mwaka 2012 vijana 300 kutoka katika makundi mbali mbali ya kijamii mjini Milano, Kaskazini mwa Italia, kupitia Bologna na Firenze walikutanika mjini Vatican na baadaye kupata fursa ya kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Tarehe 31 Mei 2014, watoto kutoka Napoli wanaoishi katika mazingira hatarishi, kiasi cha kukata tamaa ya maisha. Wakiwa mjini Roma, watoto hao watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, watatembelea Vatican na mji wa Roma katika ujumla wake. Lengo ni kuwajengea watoto hao uwezo wa kufahamiana na watoto wenzao, ili kuweza kuwa na matumaini mapya katika maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.