2014-04-09 14:33:56

Vita haina mashiko tena Syria! Amani inawezekana kwa njia ya majadiliano na upatanisho!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake siku ya Jumatano tarehe 9 Aprili 2014 amemkumbuka Marehemu Padre Frans Van der Lugt, Myesuit mwenye umri wa miaka 75, aliyeishi nchini Syria kwa takribani miaka 50, aliyeuwawa hivi karibuni humo Homs, nchini Syria. Ni Padre aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wengi, akawaonjesha watu upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, akaheshimiwa na waamini wa dini mbali mbali nchini Syria.

Baba Mtakatifu anasema, mauaji ya Padre Frans yamemsikitisha sana, kiasi cha kumkumbusha maelfu ya watu wanaoendelea kuteseka na kupoteza maisha yao nchini Syria kutokana na kinzani za kijamii pamoja na vita. Baba Mtakatifu anawakumbuka watu waliotekwa nyara huko Mashariki ya Kati, kati yao kuna Maaskofu na Mapadre ambao hadi sasa hawajulikani mahali waliko! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwarejesha watu hao katika familia na jumuiya zao.

Baba Mtakatifu anawaomba waamini kuendelea kuungana naye kwa ajili ya kuombea amani huko Syria na Ukanda mzima wa Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Serikali nchini Syria na Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanasitisha mapigano, kwani vita kwa sasa haina mashiko bali ni chanzo cha maafa kwa watu na mali zao. Haki msingi za kimataifa zinapaswa kulindwa na kuheshimiwa pamoja na kutoa huduma za afya kwa wagonjwa sanjari na misaada ya kimataifa.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahamasisha wadau wakuu katika vita inayoendelea kusababisha vifo na maafa makubwa kwa watu na mali zao kuhakikisha kwamba, wanajielekeza zaidi na zaidi katika mchakato wa kutafuta amani ya kudumu nchini Syria kwa njia ya majadiliano na upatanisho wa kitaifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.