Patriaki mstaafu Emmanuel III Delly amefariki dunia
Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa majonzi makubwa habari za kifo cha Patriaki
Mstaafu Emmanuel Delly wa tatu wa Kanisa la Babiloni ya Wakaldea, kilichotokea Jumatano
tarehe 9 Aprili 2014, huko San Diego, Calfonia, nchini Marekani. Amefariki dunia
akiwa na umri wa miaka 87 na Ibada ya mazishi inafanyika Jumamosi, tarehe 12 Aprili
2014 huko Detroit, Marekani.
Katika salam zake za rambi rambi kwa Patriaki
Louis Raphael Sako wa kwanza, Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wote walioguswa
na msiba huu, uwepo wake wa karibu kwa waamini wote wanaoishi ndani na nje ya Iraq.
Marehemu Patriaki mstaafu alikuwa ni kiongozi aliyejitoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya watu wake; akahimiza watu kuheshimiana na kutendeana kwa haki na amani sanjari
na kukuza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali.
Baba Mtakatifu
anasema, anaungana na wote wanaoomboleza msiba wa Patriaki mstaafu Emmanuel Delly
wa tatu na kwamba, anaiombea roho ya marehemu ipate kuonja huruma na upendo wa Mwenyezi
Mungu, ili iweze kupumzika kwa amani.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu
wa Vatican naye pia ametuma salam zake za rambi rambi kutokana na msiba huu mzito
uliolikumba Kanisa. Historia ya maisha yake inaonesha kwamba, Marehemu Patriaki Emmanuel
Delly wa tatu alizaliwa tarehe 27 Septemba 1927. Baada ya masomo na majiundo yake
ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 21 Desemba 1952. Tarehe 19 Aprili
1963 akawekwa wakfu kuwa Askofu na kushiriki katika Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa
Pili wa Vatican.
Tarehe 6 Mei 1967 akateuliwa kuwa ni Askofu mkuu wa jimbo
kuu la Kaskar na msaidizi wa Patriaki wa Babiloni ya Wakaldei hadi tarehe 24 Oktoba
2002, alipong'atuka kutoka madarakani kutokana na umri.