Kisiwa cha Lampedusa, kilicho Kusini mwa Italia kimekuwa maarufu sana sehemu mbali
mbali za dunia kutokana na ukweli kwamba, hapa ndipo kituo kikuu cha matumaini ya
wakimbizi na wahamiaji kutoka Afrika wanaotafuta nafuu na maboresho ya maisha yao
Barani Ulaya, lakini kwa bahati mbaya, wengi wao wanafariki dunia hata kabla ya kufika
Ulaya!
Wananchi wa Lampedusa wametengeneza Msalaba ambao umebarikiwa na Baba
Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Siku ya Jumatano, tarehe 9 Aprili 2014
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Msalaba huu ni mabaki
ya mitumbwi na mashua zilizozama majini au kutelekezwa kwenye ufuko wa bahari, Kusini
mwa Italia. Msalaba utatembezwa nchini Italia, ili kusambaza ujumbe wa mshikamano
na amani kati ya Jumuiya, Parokia, Tamaduni, Miji na watu wa imani mbali mbali.
Msalaba
huu baada ya kutembezwa kwenye Parokia mbali mbali nchini Italia hatimaye, utatunzwa
kwenye Kanisa la Mtakatifu Stefano, Jimbo kuu la Milano, Italia. Msalaba huu ni changamoto
ya mshikamano wa sala na mapendo kwa wakimbizi na wahamiaji wanaopoteza maisha yao
kwa kufa maji baharini, hata kabla ya kufika kwenye "Nchi za ahadi, zilizojaa asali
na maziwa"