Taifa la Guinea Afrika Magharibi linapambana na Changamoto ya virusi vya ebola,
ambako mpaka sasa watu zaidi ya mia wamefariki dunia kwa virusi hivyo . Shirika la
Afya la dunia limeeleza katika ripoti yake kwamba hii ni changamoto kubwa wanayopambana
nao na inaweza ikawachukua kipindi cha miezi minne kuidhibiti.
WHO, inathibitisha
kwamba watu 101 wamefariki Guinea na wengine 10 nchini Liberia kwa maradhi haya ambayo
huua kati ya asilimia 25 hadi 90 kwa watu wanaoshikwa na virusi hivi vya ebola.
WHO
inatahadharisha kwamba kipindi cha kati ya kuingiwa na mwanzo wa dalili, kinategemea
hali ya afya ya mtu mwenyewe , baadhi huchukua muda mfupi kama siku mbili na wengine
huchukua muda mrefu hata wiki tatu yaani siku 21. Hata hivyo , dalili za ugonjwa
huu , kwa kawaida huanza siku minne hadi sita baada ya kuambukizwa ugonjwa huo. Dalili
za kawaida ni kama: Kujisikia kuumwa na koo ,kuwa na homa, kikohozi kikavu cha kukatikakatika,
udhaifu wa mwili , kuumwa vikali na kichwa, na misuli ya mwili, kuhara –kutoka mwa
maji mwilini, pamoja na maumivu ya tumbo na kutapika.
Pia Upele, kwikwi, macho
mekundu, na kutokwa na damu ndani na nje ya mwili, huonekana kwa baadhi ya wagonjwa.
Rangi ya ngozi huvia na kuwa nyeusi , na mara nyingi upele hauonekani hadi hapo ngozi
itakapoanza kuchunuka.
Kwa wanawake wajawazito, dalili za kawaida Ebola virusi
huwa ni pamoja na kutokwa na damu nzito na mimba kutoka. Kifo kwa kawaida hutokea
wakati wa wiki ya pili ya dalili. Waathirika kawaida wanakufa kutokana na kuwa na
upungufu mkubwa wa damu.