Kanuni msingi katika kudumisha majadiliano ya kidini
Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini hivi
karibuni alifanya ziara ya kichungaji nchini Benin, iliyoongozwa na kanuni zifuatazo:
kujionea mwenyewe, kusikiliza kwa makini, kuelewa na kuwatia moyo wadau mbali mbali
katika mchakato wa majadiliano ya kidini.
Akiwa nchini
Benin, Kardinali Tauran alifanikiwa kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa,
Serikali na waamini wa dini mbali mbali walioonesha utashi wa kujenga na kudumisha
misingi ya majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Benin
na Afrika katika ujumla wake.
Baraza la Maaskofu Katoliki Benin limefafanua
mipango na mikakati yake ya kichungaji katika mchakato wa majadiliano ya kidini pamoja
na harakati zinazofanywa na Kanisa katika kuwatangazia watu Injili ya Furaha kama
anavyosisitizia Baba Mtakatifu Francisko. Serikali ya Benin imefafanua mikakati inayotekelezwa
katika kukuza na kudumisha amani na utulivu nchini humo kwa kuwahusisha wananchi wote
wa Benin.
Kardinali Tauran amesikiliza maoni, changamoto na ugumu wanaokabiliana
nao katika utekelezaji wa mikakati hii katika uhalisia wa maisha. Jumuiya ya Seminari
kuu ya Benin imeelezea jinsi ambavyo hata katika dini asilia za Kiafrika, waamini
hao wanaweza kuona kile kilicho kweli na kitakatifu kama ambavyo Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican wanavyokazia katika Waraka wake kuhusu majadiliano ya kidini
na waamini wa dini mbali mbali duniani. Jumuiya hii imeonesha jinsi ambavyo Kanisa
nchini Benin linavyokabiliana na changamoto mbali mbali katika mchakato wa utamadunisho
wa tunu msingi za Kiinjili Barani Afrika.
Kardinali Tauran amepata fursa ya
kujionea kwa macho yake mwenyewe amani na utulivu miongoni mwa wananchi wa Benin,
kama nyenzo msingi ya maendeleo na ustawi wa wengi. Katika makala yaliyoandikwa kwenye
Hazeti la L’Osservatore Romano na Padre Chidi Denis Isizoh, Afisa kutoka Baraza la
Kipapa la Majadiliano ya Kidini anasema kwamba, kuna maneno makuu manne yanayopaswa
kuwa ni msingi wa majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali.
Maneno haya ni: kuheshimiana, kufahamiana, kupendana na kuelewana. Maneno haya yakimwilishwa
katika uhalisia wa maisha, amani na utulivu vinaweza kudumishwa miongoni mwa watu
wa mataifa.
Kardinali Tauran alipata fursa pia ya kutembelea Mlango wa Ukombozi
na Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Hapa ni mahali ambapo Wamissionari
wa kwanza waliojitosa kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu wanapumzika katika
usingizi wa amani. Akiwa katika eneo hili, Kardinali Tauran ametembelea pia kaburi
la Hayati Kardinali Bernardin Gantin, Mwafrika wa kwanza kupewa dhamana ya kuongoza
Baraza la Kipapa la haki na amani na hatimaye, kuwa ni Dekano wa Makardinali.
Kardinali
Tauran akiwa Seminari kuu ya Mtakatifu Gallo mjini Ouidah, alipata nafasi ya kuzungumza
na Majandokasisi wanaojiandaa kwa maisha na wito wa Kipadre ndani na Nje ya Benin.
Amekazia umuhimu wa majiundo makini: kiroho, kimwili, kiakili, kiutu na kichungaji,
yatakayowasaidia kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa moyo mkuu katika kipindi hiki
cha Uinjilishaji Mpya, ambacho kinadai ushuhuda wa maisha adili na utakatifu wa maisha.
Kardinali
Tauran amewashukuru wadau mbali mbali wanaoendelea kujielekeza katika mchakato wa
Majadiliano ya Kidini, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, udugu
na mshikamano wa kitaifa. Kanisa litaendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa
dini mbali mbali duniani kama sehemu ya utekelezaji wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na mchakato wa utamadunisho wa tunu msingi za Kiinjili
Barani Afrika.