Jumuiya ndogo ndogo za kikristo ni chombo cha Uinjilishaji Mpya
Baraza la Maaskofu Katoliki Korea linaendelea kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya hija
ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo mwezi Agosti, 2014, kama sehemu
ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Barani Asia. Katika mwelekeo huu, Maaskofu wamechapisha
mwongozo utakaoisaida Familia ya Mungu nchini Korea kutambua moyo, sheria na kanuni;
uzoefu na mang'amuzi ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo mintarafu changamoto za mikakati
ya shughuli za kichungaji sanjari na utekelezaji wa Uinjilishaji Mpya.
Jumuiya
ndogo za Kikristo ni shule ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili, upendo
na mshikamano wa kidugu. Nchini Korea, Jumuiya hizi zilianza kushika kasi kunako miaka
1990 na kwamba, matunda yake yamekuwa ni kikolezo kikuu katika kukabiliana na changamoto
za Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia,
nchini Korea na Asia katika ujumla wake. Uimarishaji wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo
wanasema Maaskofu Katoliki Korea ni kutaka kujenga mshikamano wa dhati miongoni mwa
Familia ya Mungu.
Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zimepata umaarufu mkubwa
Amerika ya Kusini na Barani Afrika, hususan katika Nchi za AMECEA ambako zinapewa
kipaumbele cha pekee kama sehemu mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, zinazopania
Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Jumuiya ndogo
ndogo za Kikristo zimekuwa kweli ni vitalu vya sala, tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa
katika matendo ya huruma.
Ni nyenzo muhimu sana katika Uinjilishaji mpya hata
katika azma ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha unaotolewa
na waamini walei. Nchini Korea, kwa takribani miaka ishirini, Maaskofu wameendelea
kuanzisha na kuimarisha Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo kama sehemu ya mikakati ya
shughuli za kichungaji kwa Kanisa nchini Korea.
Waamini nchini Korea wanaendelea
kusubiri kwa hamu hija ya kichungaji itakayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia
tarehe 14 hadi tarehe 18 Agosti 2014.