Huduma ya Mashemasi isindikizwe kwa sala na mashauri ya Kiinjili
Umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Jumamosi, tarehe
5 Aprili 2014, ulishuhudia Majandokasisi kumi na mmoja kutoka Shirika la Bikira Maria
wa Mlima Karmeli wakipewa Daraja Takatifu la Usemasi wa Mpito katika Ibada ya Misa
Takatifu iliyoongozwa na Askofu Anders Arbolieus kutoka Jimbo Katoliki la Stockholm,
Sweden, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Pancras, Roma.
Askofu Anders anasema,
Kanisa lilikuwa na kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuliwezesha kupata Mashemasi
wapya kumi na mmoja, kwani hawa ni matunda ya mbegu ya miito mitakatifu iliyopandwa
ndani ya Kanisa na sasa inaanza kuzaa matunda, ambayo ni sehemu ya furaha ya Pasaka
ya Kristo, hata kama bado Kanisa linaendelea na hija ya Kipindi cha Kwaresima.
Askofu
Anders anasema, huduma ni dhana inayopaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha na
vipaumbele vya watu. Mashemasi wanapaswa kutambua kwamba, wao ni watu wa huduma wanaoongozwa
na mwanga wa Kristo mwenyewe aliyekuja kuhudumia na wala si kuhudumiwa na kuyatoa
maisha yake, ili yawe ni fidia ya wengi. Hii ndiyo changamoto inayoendelea kutolewa
na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro.
Ushemasi ni Daraja la Huduma inayopaswa kugusa undani wa maisha ya watu,
kwani Yesu mwenyewe, alionesha ushuhuda huu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.
Huduma ya Mashemasi haina budi kujikita katika maisha ya sala na tafakari ya kina,
inayomwilishwa katika matendo na maisha adili. Sala iwawezeshe Mashemasi kujenga na
kudumisha umoja na Kristo. Wajitahidi kuwasaidia watu kugundua umuhimu wa maisha yao
kuwa ni wimbo wa sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wasaidiwe kugundua wito
na utume wao wa kinabii kwa kuumwilisha katika mazingira kwa njia ya huduma makini
kwa wote wanahitaji msaada wao.
Mashemasi wapya wanachangamotishwa kuwasaidia
waamini kuweza kufungua macho ya mioyo yao ili kutambua uwepo endelevu wa Kristo kati
yao, mwaliko wa kumtafuta kwa ari na moyo mkuu. Dhana ya huduma ioneshwe kwa kuzunguka
Altare, kwani pasi ya huduma, maisha ya Kikristo ni tasa. Kanisa linaweza kupata waamini
wengi, ikiwa kama litajielekeza katika huduma makini inayosimikwa katika unyenyekevu
na unyofu wa moyo! Kwa njia hii, watu watamwona Kristo kati yao na kuweza kumpokea.
Huduma ya Kanisa isindikizwe kwa njia ya Sala na Mashauri ya Kiinjili.
Mashemasi
wa Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli wanachangamotishwa kuhakikisha kwamba,
wanajikita katika umoja na mshikamano kama njia ya kuonjeshana upendo unaobubujika
kutoka kwa Kristo. Kwa njia hii, Mashemasi wanaweza kuwa ni mashahidi hai wa uwepo
endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Huyu ndiye Kristo aliyekuja kuhudumia kwa kuyamimina
maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi. Askofu Anders Arbolieus amewaomba waamini
na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza Mashemasi wapya kwa njia ya Sala na
Majitoleo yao.