Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Jumapili iliyopita, tarehe 6 Aprili 2014, limekutana
na kusali pamoja na watanzania wanaoishi mjini Roma pamoja na viunga vyake. Mara baada
ya Misa Takatifu, Maaskofu, watanzania pamoja na marafiki wa Tanzania walikaa "mkao
wa kula" ili kubadilishana mawazo.
Askofu mkuu
Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha Tanzania, amewataka watanzania wanaoishi na
kusoma mjini Roma kujenga na kudumisha msingi wa umoja na udugu kwa kusaidiana na
kuimarishana kiimani, ili wakisha imarika wao, waweze pia kuwaimarisha Maaskofu na
waamini wengine nchini Tanzania. Amewataka kuzingatia malengo yaliyowaleta Ughaibuni
na mara wanapomaliza mkataba wao basi, warejee nchini Tanzania ili kushiriki katika
ujenzi wa Ufalme wa Mungu.
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania amewashukuru watanzani kwa kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu,
Jumapili ya tano ya Kipindi cha Kwaresima iliyowashirikisha matendo makuu ya Mungu
katika kutoa, kulinda na kutetea zawadi ya uhai. Anasema, kuna michakato mbali mbali
inayoendelea nchini Tanzania, lakini kwa sasa mchakato mkubwa unaogusa akili na miyo
ya watu ni ule wa Katiba Mpya.
Askofu Ngalalekumtwa amewataka watanzania kuombea
amani, kwani hali si shwari sana mjini Dodoma, ili Katiba itakayopatikana iwe ni kwa
ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Amewatakia watanzania wote maandalizi
mema kwa ajili ya Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka ya Kristo na Pasaka ya kila mwamini.
Kwa
upande wake, Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya
Kimissionari ya Kipapa, amewataka watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma kuendeleza
umoja na mshikamano wa kidugu, kwani umoja miongoni mwa watanzania ni sehemu ya vinasaba
vyao. watu wengi wanatamani na kuumeza mate umoja na mshikamano wa watanzania. Amewashukuru
na kuwapongeza Maaskofu Katoliki kutoka Tanzania kwa kukubali mwaliko na kushiriki
na watanzania wenzao walioko Ughaibuni, Ibada ya Misa Takatifu sanjari na mkao wa
pamoja