Msalaba ni kielelezo cha Fumbo la huruma na upendo wa Mungu
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake Jumanne, tarehe 8 Aprili 2014 kwenye
Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican anasema, hakuna Ukristo pasi
na Msalaba na kwamba, hakuna mtu anayeweza kujikomboa mwenyewe kutoka katika utumwa
wa dhambi na mauti. Msalaba ni kielelezo cha Fumbo la upendo na huruma ya Mungu na
wala si pambo Kanisani.
Waisraeli walimlalamikia Mungu katika safari yao kuelekea
kwenye Nchi ya ahadi, na huko Jangwani wakaoneshwa che mtema kuni, wakaumwa na nyoka,
kielelezo cha uwepo wa dhambi katika maisha ya mwanadamu. Ni nyoka huyu huyu aliyeleta
kizaazaa kule kwenye Bustani ya Heden, alipopandisha dhambi na kuonekana kuwa ni kielelezo
cha ushindi, lakini akashushwa na kulaaniwa kiasi cha kutembelea tumbo!
Baba
Mtakatifu anasema, Yesu alipoinuliwa pale juu Msalabani, ameonesha ushindi dhidi ya
dhambi na kifo; akaonesha kwamba, Kristo ni mwana wa mtu, Masiha na mkombozi wa mwanadamu,
dira na mwelekeo wa maisha ya Kikristo yanayofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Yesu
aliyenyanyuliwa juu ya Msalaba, ni nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni Mungu
kweli na mtu kweli; aliyejinyenyekesha hata mauti ya Msalaba, ili kumkomboa mwanadamu
kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hatimaye, kumwonjesha huruma na upendo wa
Mungu usiokuwa na kifani.