Maandalizi ya mkutano mkuu wa AMECEA yanazidi kupamba moto
Wajumbe wa Bodi ya Kamati Tendaji ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
Mashariki na Kati, AMECEA katika kikao chake kilichofanyika hivi karibuni, mjini Lilongwe,
Malawi, kuanzia tarehe 10 – 13 Machi 2014, wameridhika na maandalizi yanayofanywa
na Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi kwa ajili ya Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa
AMECEA utakaofanyika mjini Lilongwe, Malawi kuanzia tarehe 16 – 26 Julai 2014.
Waamini
na watu wenye mapenzi mema nchini Malawi wanaendelea kuonesha ukarimu wao kwa kuchangia
kwa hali na mali katika mchakato unaolenga kufanikisha mkutano mkuu wa AMECEA. Wanaendelea
kusubiri kwa hamu na shauku kubwa ili waweze kushiriki katika tukio hili la kihistoria
linaliwakusanya Maaskofu na wajumbe mbali mbali kutoka katika nchi wanachama wa AMECEA.
Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi
na Serikali ya Malawi, ili kuhakikisha kwamba, tukio hili linakuwa ni kwa ajili ya
mafao na ustawi wa wananchi wengi wa Malawi. Waamini wanaendelea kusali kwa ajili
ya kumwomba Roho Mtakatifu aweze kufanikisha tukio hili. Sala ya kuombea mkutano mkuu
wa AMECEA itatumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki AMECEA ili iweze kutawanywa
Majimboni, Parokiani na Vigangoni, ili kutoa nafasi ya waamini pia kushiriki kikamilifu
katika tukio hili la maisha ya kiroho.
Padre Ferdinand Lugonzo, Katibu mkuu
wa AMECEA anasema, Sekretarieti ya AMECEA inaendelea pia kukusanya mchango kutoka
kwa nchi wanachama na wadau mbali mbali kwa lengo hili. Kwa upande wake, Askofu mkuu
Tarcisio Zizaye, Mwenyekiti wa AMECEA amewashukuru Makatibu wakuu kutoka katika nchi
za AMECEA katika utekelezaji wa majukumu yao. Amewataka kuhakikisha kwamba, wanafanikisha
mkutano huu ambao ni kielelezo cha ushirikiano, mshikamano, umoja na udugu miongoni
mwa Maaskofu wa AMECEA.