Kanisa linapania kushiriki kikamilifu katika kudumisha amani na majadiliano ya kidini
huko Mashariki ya Kati!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni tarehe 7 Aprili 2014 amekutana na kuzungumza
na Mfalme Abdullah wa Pili wa Yordan pamoja na ujumbe wake, ambao walipokelewa na
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, aliyekuwa ameandamana na viongozi
kadhaa kutoka Vatican.
Baba Mtakatifu na mgeni wake wamefanya mazungumzo yao
kwenye Hostel ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican. Mazungumzo haya kadiri ya
taarifa ya Padre Lombardi yamefanyika wakati viongozi hawa wawili wakiwa wanaendelea
kupata chai ya jioni na kwamba, yamedumu kwa takribani dakika arobaini na tano.
Safari
ya kikazi iliyofanywa na Mfalme Abdallah wa pili mjini Vatican ni sehemu ya maandalizi
ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko huko katika Nchi Takatifu, ambako
atapata fursa kwanza kabisa ya kutembelea na kuzungumza na wananchi wa Yordan na kwamba,
wananchi wengi wa Yordan wanasubiri kwa hamu hija hii ya kichungaji, itakayomwezesha
Baba Mtakatifu kujionea hali halisi ya wananchi wa Yordan.
Kwa upande wake,
Baba Mtakatifu ameonesha utashi na nia ya kimaadili ya kutaka kushiriki kikamilifu
katika mchakato unaopania kupata amani ya kudumu huko Mashariki ya kati pamoja na
kudumisha majadiliano ya kidini, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Mwishoni,
Baba Mtakatifu amesalimiana na wajumbe waliokuwa kwenye msafara wa Mfalme Abdallah
wa pili wa Yordan.