2014-04-07 08:03:10

Toba, msamaha na upatanisho ni mambo yanayohitaji kifua kipana!


Mpendwa Msikilizaji wa Radio Vatican, Tumsifu Yesu Kristo! Kwa siku hizi arobaini, pamoja na Mama Kanisa, tupo jangwani, tunasali, tunafunga, tunatoa sadaka na tunashughulikia kwa uzito zaidi wongofu wa mwenendo wetu. RealAudioMP3

Tunakiri udhaifu wetu mbele ya Mungu na mbele za wanadamu wenzetu; tunaomba huruma ya Mungu na msaada wa sala za ndugu zetu, zitusaidie kuinuka na kuendelea mbele katika safari yetu ya kumjua Mungu, kumpenda na mwisho kufika kwake.

Mpendwa msikilizaji, baada ya kuona kwa uchache juu ya hali yetu ya dhambi, leo tuangazie juu ya tunu ya toba, msamaha na kujirekebisha. Kama ambavyo tunakiri mapungufu yetu na kuomba huruma ya Mungu atusamehe, papo hapo, kwa mwangwi wa ile sala ya aliyotufundisha Bwana, sisi nasi tunaomba neema ya kuwasamehe waliotukosea (mt. 6:12), na pia tunaomba neema ya kuupokea msamaha na kurekebisha makosa yetu.

Tunapotubu kwa moyo kabisa kadiri ya taratibu za Kanisa, Mungu mwenye huruma anatusamehe makosa yetu. Tunapoomba radhi kwa wenzetu, nao pia wakitusamehe, ni huruma ileile ya Mungu inakuja kwetu kwa njia ya zawadi ya msamaha tunaoupokea kutoka kwa wenzetu. Kwa mwangwi huo, tujihekimishe neno hili, kusamehe ni kuwa chombo cha huruma ya mungu. Mungu anapendezwa na mwanadamu aliye tayari kusamehe. Mungu anatukuzwa katika kutusamehe sisi makosa yetu (tukitubu kwa moyo) na anatukuzwa pia katika kusameheana kwetu.

Mpendwa msikilizaji, katika Jumatano ya majivu neno la Mungu lilitualika sote kufanya TOBA. Kwa leo tuitazame toba kwa namna mbili. Kwanza toba kama tendo la kawaida kabisa la mwanadamu na pili, toba kama Sakramenti kadiri ya mafundisho-imani ya Kanisa letu. Katika hilo la kwanza, kwa kufuata fundisho la Bwana (Mt. 18:22) tunataka kusema, mtu ukimkosea mwenzako, uwe muungwana tu, jipe moyo; nenda kamwombe msamaha. Usikomae na kujisahaulisha kosa lako. Kuomba radhi ni tendo la kiutu na ni ujasiri pia. Kuzungumza na kuomba msamaha kunatupatia nguvu ya kujenga mahusiano mema.

Na sehemu ya pili tunaitazama toba kama Sakramenti. Tukitenda dhambi, tunatubu/tunaungama kwa moyo wa unyoofu wote. Sakramenti ya Kitubio ni sakramenti ya Upatanisho. Tunajipatanisha na nafsi zetu, na binadamu wenzetu na zaidi kabisa tunajipatanisha na Mungu. Sakramenti ya kitubio ni safari ya maamuzi, mapokezi na sherehe ya Mwana mpotevu anayerudi nyumbani kwa baba.

Na huko nyumbani kwa baba, huyu mwenye kutubu, anavikwa vazi la neema aliyoipoteza kwa dhambi, anavikwa viatu kuonesha kuwa amekuwa huru akilini, mwilini na rohoni, mwana huru wa Mungu, na anavikwa pete kuonesha muungano wake na familia ya Baba mwema. Kwa mwangwi wa uelewa huo, tunafundishwa juu ya uzito na mafaa ya sakramenti ya Kitubio, sakramenti ya Utakaso na Upatanisho. Tuipende na tuikimbilie daima kwani ndipo tunapoguswa nafsi zetu kwa huruma ya Mungu, ndipo tunaporudishiwa hadhi kwa neema ya utakaso.

Wengi wetu ni majasiri kutenda dhambi, lakini ni waoga sana kutubu. Matokeo yake tunadhoofika akilini, mwilini na rohoni. Mzaburi anasema ‘nilipoficha dhambi, mifupa yangu ilidhoofika na nyama yangu ikaungulia kama kwenye joto la Kaskazi...’. Dhambi hudhuru mwili na roho pia. Katika kipindi hiki cha kwaresma tunaposhughulikia wongofu wetu, tunataka kwa roho ya uwazi na ukweli tujipime na tujiwekee mkakati kama mwana mpotevu – jasiri tuseme, nitaondoko, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia...!

Kama Baba Mtakatifu Francisko anavyotuhimiza daima, Mungu mwenye huruma anatusubiri turudi kwake, yupo tayari kutusamehe, yeye kamwe hachoki kutusamehe, ni sisi ndiyo tunachoka na tunaona aibu kurudi kwake.Ewe ndugu mpendwa, tutaishi katika dhambi MPAKA LINI? Amua sasa kwani wakati uliokubaliwa ndio sasa, wakati wa wokovu ndio huu... (2 Kor 6 : 2 ).

Kama ambavyo sisi tungependa kusamehewa na Mungu, ni sharti kwanza tuwe tayari kuwasamehe wale waliotukosea. Katika sala ya Bwana tunasali ‘utusamehe makosa yetu, kama sisi tunavyowasamehe waliotukosea’. Mara nyingi tunaomba huruma ya Mungu wakati sisi HATUTAKI KABISA, kuwasamehe waliotukosea hata kama wanatuomba msamaha. Kwa baadhi yetu, kwa nini kusamehe ni kugumu?? Ili tuweze kusamehe, lazima kwanza tuombe nguvu ya Mungu. Mungu mwenye kutuumbia mioyo safi atusaidie. Na pili lazima kuamua kusamehe.

Wakati mwingine tunafanya TENDO LA MSAMAHA bila KUAMUA kusamehe na bila nguvu ya Mungu. Matokeo yake, tutafanya vikao vingi vya kupatanishana na tutapeana zawadi na kadi nyingi za samahani, lakini vinyongo vinabaki, kumbukumbu mbaya ya maumivu, hasira na chuki inarudi mara nyingi! Hiyo ni kwa sababu HUKUAMUA KUSAMEHE, Ulitamka tu maneno ya kusamehe. Wengine tunahalalisha kutokusamehe kwetu kutokana na uzito wa makwazo tuliyotendewa! Ndugu yangu, hata kama umekosewa vipi, Msamaha unawezekana, KUSAMEHE INAWEZEKANA. Tuone mifano michache kutoka katika maandiko matakatifu ya watu waliokanyagwa haswa, lakini WALISAMEHE.

ESAU ANAMSAMEHE YAKOBO Esau akaja mbio kumlaki Yakobo, akamkumbatia na kumwangukia shingoni akambusu, nao wakali sana. Mwa. 33:4 . YOSEFU A NAWASAMEHE NDUGU ZAKE! ‘... akasema Basi sasa msihuzunike wala kufadhaika kwa kuniuza. Mungu ndiye aliyenileta huku niwatangulie ili niyaokoe maisha ya watu. Akiwa bado analia, Yosefu aliwakumbatia ndugu zake na kuwabusu. Hapo ndipo ndugu zake walipoweza kuzungumza naye. Mwa. 45: 5, 15. Yosefu anatufundisha kuona mpango wa Mungu hata katika mambo mabaya.

BABA MWEMA ANAMSAMEHE MWANA MPOTEVU. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkumbatia na kumbusu. Lk. 15: 20b. Hata YESU ALIWASAMEHE WATESI WAKE, Lk. 23:34. Yesu akasema ‘Baba, uwasamehe kwani hawajui watendalo’. Maandiko matakatifu pia yatuelekeza kusamehe. Tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, tena wenye huruma, mkasameheane. [Ef. 4:32]. Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu ana jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe ninyi [Kol. 3:13].

Ndugu yangu akinikosa, nimsamehe mara ngapi? Hata mara saba? Yesu akamwambia, sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. [Mt. 18:22]. Na tukisha kusamehewa, tuwe tayari kurekebisha makosa yetu. Haileti maana kutubu huku unaendelea kutenda kosa lilelile tena kwa ushupavu zaidi. Kufanya toba ni kuwa tayari kufanya mabadiliko.

Uradhi wetu na nguvu ya Mungu vitusaidie. Kurekebika ni kuheshimu huruma ya Mungu, kusahihisha makosa yetu ni kuwaheshimu wale waliotusamehe. Mungu atujalie ujasiri wa kweli, tufanye toba ya kweli, na tuziache njia zitupelekazo upotevuni.

Kutoka Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.