Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo la Rulenge-Ngara ambaye pia ni Makamu wa Rais,
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican wakati
wa hija yao ya kitume mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 8 Aprili 2014 anasema
kwamba, Tanzania katika kipindi cha miaka 50 imepita katika hatua kuu mbili; Tanzania
iliyokuwa imejengeka katika mshikamano na umoja wa kitaifa kwa kuzingatia mawaidha
na ushauri wa wasisi wa taifa la Tanzania.
Awamu ya
pili ya Tanzania inajionesha kwa namna ya pekee mara baada ya kuingia kwa vyama vingi
vya kisiasa, hali ambayo inaonesha mpasuko na misigano kati ya watanzania.
Askofu
Niwemugizi anasema, changamoto ni sehemu ya hija ya maisha ya mwanadamu na kamwe haziwezi
kukosekana mahali popote pale. Watanzania licha ya umaskini wao, kwa miaka mingi waliendelea
kushikamana kama ndugu na kukabiliana na changamoto katika medani mbali mbali za maisha
katika umoja, mshikamano na upendo; kweli watanzania walijisikia kuwa ni wamoja, kiasi
hata cha kuwajengea majirani zao “wivu mtakatifu”, kwa kuwaona jinsi walivyokuwa wanaishi
kwa amani na utulivu! Tanzania ikaonekana kuwa kama ni “Kisiwa na Amani”.
Uwepo
wa vyama vingi vya Kisiasa nchini Tanzania, zilikuwa ni dalili za kukomaa kwa siasa
na demokrasia kati ya watanzania, lakini ni mchakato uliobeba changamoto nyingi katika
maisha ya watanzania wengi. Umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa watanzania
ukaanza kuchechemea na watanzania wakaanza kubaguana kwa kufuata itikadi za vyama
vyao vya kisiasa, dini na mahali anapotoka mtu. Mivutano na utengano miongoni mwa
watanzania vikaanza kushika kasi ya ajabu! Hii inatokana na ukweli kwamba, bado hakuna
ukomavu wa kutosha katika vyama vya kisiasa, kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi,
umoja, ustawi na maendeleo ya watanzania wote.
Askofu Niwemugizi anasema mchakato
wa Katiba Mpya ya Tanzania uliwaonjesha watanzania matumaini mapya kwa kuwa na Katiba
Mpya, ambayo kimsingi ni sheria mama. Hapa mpasuko na mgawanyiko wa watanzania: kisiasa
na kidini vikajionesha kwa namna ya ajabu kabisa, kila upande unajitahidi kuvutia
kwake, umoja wa kitaifa inaonekana kana kwamba, unawekwa rehani!
Askofu Niwemugizi
ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anakiri kwamba,
hata ndani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania sauti ya kinabii iliyokuwa na nguvu
wakati fulani, imeanza kufifia kutokana na woga wa kupachikwa misimamo ya kisiasa
hata kama kimsingi Kanisa halina Chama cha Kisiasa. Askofu Niwemugizi anasema, kuna
haja kwa watanzania kuanza tena kwa kasi na ari mpya mchakato wa kujenga na kuimarisha
umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kutafuta na kusimamia haki msingi za binadamu,
mafao ya wengi na ustawi wa watanzania wote!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.