Miaka 20 tangu yalipotokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda
Tarehe 7 Aprili 2014, Rwanda inafanya kumbu kumbu ya miaka ishirini, tangu mauaji
ya kimbari yaliyopokea nchini humo na kusababisha maafa makubwa kwa watu wasiokuwa
na hatia, kunako Mwaka 1994. Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa
Bwana, Jumapili iliyopita kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican, amelikumbuka
tukio hili, kwa kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya maisha ya kiroho.
Papa
ametaka Wanyarwanda wote kusonga mbele kwa imani na matumaini, katika mchakato wa
upatanisho, ambao tayari unaanza kuonesha matunda makubwa. Hii ni changamoto ya kujenga
na kuimarisha umoja na mshikamano wa kiutu na maisha ya kiroho, kwa ajili ya ustawi
na mafao ya wananchi wote wa Rwanda. Baba Mtakatifu anawaalika wananchi wote wa Rwanda
kutokuwa na woga, bali wajishikamanishe na kujenga nchi yao katika misingi na kweli
za Kiinjili, katika upendo na maridhiano, ili amani ya kweli iweze kupatikana.
Baba
Mtakatifu Francisko amewaombea ulinzi na tunza ya kimama kutoka kwa Bikira Maria wa
Kibeho. Anawakumbuka Maaskofu Katoliki Rwanda waliohitimisha hija yao ya kitume hapa
mjini Vatican hivi karibuni.
Baba Mtakatifu amewakumbuka pia waathirika wa
ugonjwa wa Ebola huko Guinea na nchi jirani ambako zaidi ya watu themanini tayari
wamekwisha poteza maisha yao
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewagawia
Biblia Takatifu, waamini waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican, kama kielelezo cha kuwakabidhi Waketekumeni Neno la Mungu ili
waweze kujiandaa barabara katika Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka.