2014-04-07 12:12:34

Maaskofu wafunika Roma!


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Jumapili iliyopita, tarehe 6 Aprili 2014 kwa kushirikiana na Maaskofu Katoliki Tanzania ambao wako katika hija yao ya kitume mjini Vatican, wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Salette, Kanisa la Kitume la Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa Makleri, Watawa, Waamini walei pamoja na Wanaparokia ili kuonesha kwamba: Kanisa ni: Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume. RealAudioMP3

Mahubiri yalitolewa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza aliyekazia umuhimu wa kutubu na kumwongokea Mungu hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Neno la Mungu liwe ni mwongozo na dira ya maisha ya waamini kwa kulimwilisha katika uhalisia wa maisha, ili aweze kuwa kweli huru na kifo, dhambi pamoja na mambo yote yanayomtumbukiza katika giza na ulevegu wa maisha ya kiroho.

Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, waamini wawe huru kuchuchumilia tunu ya maisha mapya kwa kuepuka kuendelea kuwa wahanga wa dhambi na mauti, kwa kupenda kutembea kama watu huru katika njia za Bwana, pasi na kukata tamaa ya kifo, daima wakijitahidi kumrudia Mungu, ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo.

Mwanadamu anaendelea kuandamwa na magonjwa, kifo na maziko kama ilivyokuwa kwa Lazaro anayeimuliwa katika Injili ya Jumapili ya tano ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka A wa Kanisa. Yesu kama rafiki mwaminifu wa binadamu anaendelea kuwatembelea binadamu katika shida na mahangaiko yao kama alivyofanya kwa Rafiki yake Lazaro, kwani anawapenda na anataka kuwaokoa na kuwakirimia mwanga unaopaswa kupokelewa na kuthaminiwa. Yesu anataka kuwapatia rafiki zake ufufuko na maisha mapya yanayojikita katimka imani, matumaini na mapendo.

Ibada ya Misa Takatifu ilipambwa kwa nyimbo za Kwaresima zilizoimbwa vizuri na Watawa, Makleri na Waamini walei, waliokuwa wanasindikizwa kwa kinanda kilichokuwa kinatekenywa kwa ufundi na utaalam mkubwa kutoka kwa Padre Alcuin Nyirenda, OSB, hapa Waswahili wakasema, ama kweli, leo upele ulipata mkunaji! yaliyojiri baadaye, usikose kujiunga nasi tena, tutakapoendelea kukuchambulia kwa kina na mapana, hija ya kitume ya Maaskofu Katoliki Tanzania hapa mjini Vatican.

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.