2014-04-05 10:45:32

Mwalimu Julius K. Nyerere awe ni kiongozi wa mfano katika kudumisha haki na amani!


Askofu mstaafu Paride Taban wa Jimbo Katoliki la Torit, Sudan ya Kusini anawachangamotisha viongozi wa Serikali na vyama vyama vya kisiasa nchini humo kuondokana na ukabila, ubinafsi, uchu wa mali na madaraka na badala yake, wajitoe bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Sudan ya Kusini, bila upendeleo wala ubaguzi.

Askofu mstaafu Taban anasema, ukabila na udini ni sumu ya amani, maendeleo na ustawi wa wananchi wengi. Viongozi wa Serikali Sudan ya Kusini, wajitahidi kufuata mfano wa Mwalimu Julius Kambare Nyerere, Muasisi wa Tanzania aliyesimama kidete kulinda na kutetea umoja, upendo na mshikamano wa watu wake, kiasi kwamba, Tanzania ikajulikana kuwa ni "Kisiwa cha Amani". Kwake, ukabila na udini haukuwa na nafasi, mambo ambayo leo hii yanaendelea kusababisha maafa makubwa huko Sudan ya Kusini na sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

Anasema, wananchi wa Sudan ya Kusini wameteseka sana hadi wakajipatia uhuru wa bendera, miaka michache tu imepita, tena wametumbukizwa kwenye machafuko na vita ya wenyewe kwa wenyewe! Hakuna sababu ya watu kuendelea kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Umefika wakati kwa Sudan ya Kusini kujikita katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upatanisho na mshikamano wa kitaifa badala ya kuendekeza ukabila na udini, mambo yanayohatarisha mustakabali wa taifa.

Askofu Taban anasema, umefika wakati wa kutafuta suluhu ya migogoro na kinzani za kijamii kwa njia ya majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi na mafao ya wengi. Wananchi wajifunze kujenga na kudumisha haki na amani, kama masharti makuu ya kujipatia maendeleo endelevu. Wananchi wakwepe kishawishi cha kutumbukizwa katika vita kwa kuendekeza ushabiki wa kisiasa usiokuwa na mvuto wa mashiko kwa wananchi walio wengi!

Kuhusu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa Taifa, katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema kwamba, licha ya shida na mahangaiko yao, lakini wanafarijika kuona kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaendeleza mchakato wa kutaka Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aweze kutangazwa na Mama Kanisa kuwa ni kati ya wenyeheri, kama kiongozi na mfano kwa wanasiasa na waamini walei, kutokana na upendo wake kwa Kristo na Kanisa lake, mambo msingi yaliyomwezesha kuishi na kutenda kama mwanasisa na akawa kweli ni mfano bora wa kuigwa na mataifa mengine!







All the contents on this site are copyrighted ©.