Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha na kukumegea mchango uliotolewa
na Wenyeheri Yohane XXIII pamoja na Yohane Paulo II katika maisha na utume wa Kanisa
mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Leo katika makala haya tunazama zaidi katika
kupembua mchango wa Mwenyeheri Yohane XXIII.
Maana ya mafundisho
jamii ya Kanisa: Ni mkusanyiko wa mawazo na mafundisho kuhusu jamii, ambayo Kanisa
limekuwa likiyatilia mkazo, hasa kuhusiana na maswala ya haki jamii, umaskini, utajiri,
maswala ya uchumi, muundo wa jamii na wajibu wa Serikali za nchi katika kukabiliana
na maswala hayo kwenye jamii husika.
Mafundisho haya yanapata chimbuko lake
katika Waraka wa kwanza kabisa kuhusu maswala ya jamii, ulioandikwa mnamo mwaka 1891
na Papa Leo XIII, ambao unajulikana kwa jina la Rerum Novarum, “Mambo Mpya” Lakini
kwanza kabisa, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chumbuko lake katika Maandiko Matakatifu,
Maandishi na mawazo ya Mtakatifu Thomas wa Aquino na mafundisho ya Mtakatifu Augustino,
Askofu na Mwalimu wa Kanisa kuhusu maswala ya jamii. Mafundisho jamii ya Kanisa yamesimikwa
kwenye nguzo kuu tano:
Manufaa ya wote, Mshikamano, kusaidiana kwa kujikita
katika kanuni ya auni, upendeleo wa pekee kwa maskini zaidi katika jamii, mali yote
iliyopo duniani ni kwa ajili ya matumizi ya wanadamu wote. Nguzo hizi tano zinapata
chimbuko lake katika: Maandiko Matakatifu, Mapokeo ya mababa wa Kanisa na Nyaraka
mbalimbali zinazotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na zile zinazotolewa
na viongozi wa Makanisa mahalia popote duniani.
Kwa hayo maelezo mafupi, tunaweza
sasa kuona ni jinsi gani hawa mapapa wawili ambao mama Kanisa atawatangaza watakatifu,
walichangia kwa njia ya mafundisho yao katika kuendeleza Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Katika makala haya tutaanza kwa kuchambua mchango uliotolewa na Papa Yohane XXIII
katika mchakato wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu Mafundisho Jamii.
Papa
Yohane XXIII : Kanisa ni Mama na Mwalimu; Amani Duniani Angelo Giuseppe Roncalli
alizaliwa kwenye familia maskini ya wakulima huko Bergamo- kaskazini mwa Italia mnamo
tarehe 25 Novemba 1881, akiwa ni mtoto wa nne kati ya watoto kumi na watatu. Familia
yake iliishi maisha bora ya Kikristo na ilijishughulisha sana na maswala ya kanisa.
Mjomba wake mmoja Zaverio, alichangia sana katika makuzi ya kiroho na ya kiutu ya
Angelo Giuseppe Roncalli. Mjomba huyu alikuwa ni mwanaharakati wa chama cha “Catholic
Social Action” ambacho kilikuwa kimeanzishwa wakati ule na Askofu mkuu wa Jimbo kuu
la Bergamo ili kusaidia maswala ya jamii.
Hili ni jambo ambalo lilikuwa limehimizwa
sana na Papa Leo wa XIII kwenye waraka wake wa jamii Rerum Novarum au kwa lugha ya
kiswahili Mambo mapya, akimaanisha mabadiliko yaliyokuwa yanatokea kwenye Bara la
Ulaya wakati wa Mapinduzi ya Viwanda na jinsi ambavyo miundombinu hii, pamoja na kwamba,
ilikuwa ni hatua kubwa ya maendeleo, lakini iliwaathiri wafanyakazi ambao walijikuta
wakipunguzwa au kuachishwa kazi kutokana na kwamba kazi walizokuwa wakizifanya kwa
mikono, sasa kwa asilimia kubwa zilikuwa zinafanyika kwa mashine na hivyo uwepo wao
katika viwanda haukuonekana tena kuhitajika.
Jambo hili lilisababisha umaskini
mkubwa wa hali na kipato katika jamii licha ya mabadiliko yaliyotokea katika sekta
ya uchumi na maendeleo. Mambo haya yalikuwa yanatokea hata nchini Italia, na ndiyo
maana, jimbo la Bergamo lilikuwa linajitahidi kuganga machungu ya watu waliokuwa wanaendelea
kuathirika kutokana na mabadiliko hayo.
Baada ya kupewa Daraja la Upadre,
Padre Angelo Roncalli alifanya utume waka katika hospitali kama mhudumu wa kiroho.
Vile vile, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia alikuwa akitoa huduma za kiroho kwenye
kambi za kijeshi. Yale aliyoyaona kutokana na matukio yale yalimfanya aamini kwamba
“ kwa kweli vita ni shetani mkubwa”. Kazi zake za kitume zilimlazimu kutoka nje ya
Italia.
Historia ya maisha yake inaonesha kwamba, kuanzia mwaka 1924 hadi
1934 Padre Angelo Roncalli alikuwa mwakilishi wa baba mtakatifu katika nchi ya Bulgaria.
Na kuanzia mwaka 1934 – 1944 alikuwa mwakilishi wa Papa katika nchi ya Uturuki na
Ugiriki. Katika nafasi hizi za kitume, aliweza kukuza muono wa kiekumene na ule wa
majadiliano na watu wa imani mbalimbali. Mwisho mwa mwaka 1944 padre Angelo Roncalli
aliteuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Ufaransa. Akiwa katika wadhifa huo huko Ufaransa,
alikuwa pia Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa. Akiwa katika
utume huu alijifunza kwamba, inawezekana kabisa kuweka pembeni tofauti za misimamo
ya kisiasa ambazo na kufanya “mazungumzo na watu wote wenye mapenzi mema”.
Katika
uhusiano wake na wale ambao hawakuwa na imani Katoliki, alijaribu kuangalia zaidi
mambo yale yanayouwanganisha na Wakatoliki, zaidi kuliko kuangalia yale yanayowatenganisha.
Hii ikawa ni chemchemi ya majadiliano ya kiekumene na kidini; mambo yaliyovaliwa njuga
na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na bado yanaendelea kupewa kipaumbele
cha pekee na Kanisa Katoliki katika maisha na utume wake, ili dunia iweze kuwa ni
mahali pazuri pa kuishi watu wakiheshimiana na kuthaminiana kama ndugu, licha ya tofauti
zao za kiimani, kisiasa na kitamaduni.
Mnamo mwaka 1953 aliteuliwa kuwa
askofu mkuu na patriaki wa Venice- Italia. Angelo Roncalli alichaguliwa kuliongoza
Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro mnamo tarehe 28 Oktoba 1958, mwezi
mmoja kabla ya kutimiza umri wa miaka sabini (70). Alichagua jina Yohane wa XXIII,
na aliliongoza Kanisa kwa kipindi cha miaka minne na miezi saba.
Dunia
ikiwa katika hali ya vita baridi, mwaka 1959 Papa Yohane XXIII aliutangazia ulimwendu
nia yake ya kuitisha Mtaguso Mkuu ili kuleta upyaisho (aggiornamento) katika Kanisa;
na kubadili mtazamo wa Kanisa kuelekea jamii, ili Kanisa liwe wakala wa umoja na
haki. Kadiri mipango ya kufanya mtaguso ilivyozidi kusonga mbele, ilikuwa wazi kwamba
papa angeelekeza nguvu zake kwanza kabisa kwenye maswala ya ndani ya Kanisa, yaani:
Liturujia, Utume wa Askofu mahalia, asili ya Kanisa na kadhalika.
Kwa hiyo,
tunaweza kusema kwamba, Baba Mtakatifu alikuwa na ajenda tatu katika utume wake kama
khalifa wa mtakatifu Petro. Ajenda ya kwanza ilikuwa ni upyaisho wa Kanisa, (kuleta
mabadiliko ndani ya Kanisa) “aggiornamento” jambo la pili lilikuwa ni Umoja wa Madhehebu
ya Kikristo; na jambo la tatu ni umoja na amani kati ya watu wa mataifa au amani duniani.
Mtaguso wa Kiekumene ndio ulipaswa kuleta haya mabadiliko ndani ya Kanisa Katoliki,
na baada ya hapo kutoka kifua mbele kwa ajili ya kuanza majadiliano na makanisa mengine
ya kikristo na kuingia kwenye umoja wa kiekumene.
Hali ilivyokuwa duniani wakati
wa uongozi wa Papa Yohane XXIII kama Khalifa wa Mtakatifu Petro Katika kipindi
cha uongozi wa papa Yohane wa XXIII jumuiya ya kimataifa ilikuwa inapita kwenye mabadiliko
mengi kijamii, kisiasa na kiuchumi. Itakumbukwa kwamba ni kwenye mwaka 1959 Rais Fidel
Castro na jeshi lake wanachukua madaraka huko Cuba na Havanna kwa ujumla; mwaka huo
huo John Kennedy anachaguliwa kuwa Rais wa Marekani; mwaka 1960 unaundwa Umoja wa
nchi zinazo uza na kusambaza petroli nje ya nchi zao (OPEC); mwaka huo huo Marekani
inaingia kwenye mgogoro wa kivita na nchi ya Vietnam; Ukuta wa Berlin unajengwa; mwanadamu
wa kwanza anafanya safari kwenye sayari kuizunguka dunia mnamo mwaka 1961; makombora
ya Urusi nchini Cuba yanasababisha mgogoro kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti,
mgogoro ambao ulikuwa karibu unafikia ukingoni mwa kuanza vita vya nyuklia. Ni mwaka
ambao pia nchi nyingi za Afrika, moja baada ya nyingine, zinaanza kujipatia uhuru
wa bendera kutoka kwa wakoloni.
Katika matukio haya yote, Papa Yohane XXIII
alitaka Kanisa litoe mchango wake katika kukabiliana na hali hii iliyokuwa inaukumba
dunia. Ila kwa namna moja au nyingine, Kanisa hadi kipindi kile halikuwa na mtizamo
wa kijamii na wala mchango wake haukuwa unajulikana wala kuonekana katika matukio
yote hayo. Hivyo basi, jambo la kwanza alilofanya Papa Yohane XXIII ni kulitambulisha
Kanisa kwa dunia nzima.
Baba Mtakatifu Yohane XXIII alilitambulisha Kanisa
kama "Mater et Magistra", yaani Kanisa ni Mama na Mwalimu wa mwanadamu. Kwa kulitambulisha
Kanisa kwa namna hii, Papa Yohane wa XXIII alikuwa na lengo la kulifanya Kanisa libadili
mwelekeoo lililokuwa nao hadi kipindi kile na alitaka kulitumikia kama wakala wa Umoja
wa Wakristo na kuisaidia jamii ili iweze kushughulikia maswala ya ukosefu wa haki
kwenye maswala ya uchumi, tishio la vita ya nyuklia na migogoro kati ya mataifa. MM
ilitolewa rasmi mnamo mwezi Julai 1961 mwaka mmoja na miezi mitatu kabla ya kuanza
kwa mtaguso, na PT ilitolewa wakati Mtaguso ukiendelea, yaani tarehe 11 Aprili 1963.
MM ilileta mtazamo mpya kwenye tafakari ya Kanisa juu ya masuala ya kijamii. Waraka
huu ulitolewa kwanza kabisa kwa ajili ya kuadhimisha miaka 70 ya RN.
Usikose
kumshirikisha jirani yako mchango uliofanywa na Mwenyeheri Yohane XXIII katika maisha
na utume wake mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
itaendelea kukujuza kwa kina na mapana mchango wa Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane
Paulo II, wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kujiandaa kuwatangaza kuwa ni Watakatifu,
hapo tarehe 27 Mei 2014, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro pamoja na viunga
vyake, vitakapowaka kwa moto wa furaha!