Tumekuja kusali na kuteta na Baba Mtakatifu Francisko!
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika
mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, hija ya kitume inayofanywa sasa
na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 7 Aprili 2014
ni utaratibu wa kawaida kwa Kanisa Katoliki. Hii ni hija ambayo walau hufanyika kila
baada ya miaka mitano, ili kuweza kuonana, kusali na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu
Petro.
Hii ni nafasi
ya kusali pia kwenye makaburi ya miamba wa imani: Mtakatifu Petro na Mtume Paulo,
mwalimu wa mataifa. Hawa ni mashahidi wa kazi ya utangazaji wa Habari Njema ya wokovu,
ambayo Yesu alitaka iendelezwe duniani kote. Hii ni nafasi pia kwa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania kutoa taarifa ya maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania kama
sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu na imani.
Rais
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema kwamba, hii ni fursa ya kuwashirikisha
viongozi wa Kanisa: furaha, matumaini na wasi wasi la Kanisa Katoliki nchini Tanzania.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaendelea kusukuma mbele mchakato wa kuwatangaza
Sr. Bernadetha Mbawala na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa kuwa ni
kati ya Wenyeheri.
Askofu Ngalalekumtwa anasema, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
ni mfano wa mtu ambaye kama kiongozi mkuu wa taifa, alijitahidi kuzingatia majukumu
yake, akajikita katika hekima, heshima, busara na upendo kwa wote bila ubaguzi. Chimbuko
la utekelezaji wa majukumu yote haya na maisha yake adili ni imani kwa Kristo na Kanisa
lake.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linasema, haya ni mambo yanayowatia
moyo katika shida na mahangaiko yao; wakati wa mashambulizi, dhuluma za kidini na
misigano ya kijamii, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu bado anawataka Maaskofu kuendelea
kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Wamefika kusali kwenye makaburi ya miamba
wa imani, ili waendelee kutiwa nguvu ya kuwa ni mashahidi wa Kristo nchini Tanzania
kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ana huruma na mapendo na ataweza kuwasikiliza.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania, linawaalika kwa namna ya pekee waamini na watanzania
wote kutubu na kumwongokea Mungu ili waweze kuponywa katika mapungufu yao na kupata
maisha mapya pamoja na kukumbatiwa kwa upendo, wao wakionesha moyo wa toba na majuto.