2014-04-04 14:07:57

Mchakato wa maboresho ya maisha ya watanzania


Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu Kufanyiwa Mapitio kwa kuangalia: malengo pamoja na kuangalia viashiria vya idadi ya watu.

1. Utangulizi:
Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu kwanza ya iliandaliwa mwaka 1992 ambapo ilifanyiwa na kuandaliwa upya mwaka 2006 kwa azma ya kuratibu na kushawishi sera za sekta nyingine, mikakati na program za maendeleo kuhakikisha zinajumuisha masuala ya maendeleo endelevu ya watu, kukuza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake, haki za watoto, na makundi mengine yenye uwezekano wa kuathiriwa kwa urahisi.

Tangu mwaka 2006 hadi sasa, maendeleo mapya yametokea kitaifa na kimataifa yenye uhusiano wa moja kwa moja na masuala ya idadi ya watu na maendeleo, mfano masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, Magonjwa yasiyo ya kuambukiza, nk. Kimataifa kumekuwepo na msukumo mpya wa kuimarisha maendeleo endelevu ya masuala ya idadi ya watu mfano masuala ya diaspora, mabadiliko ya tabia nchi, uhaba wa chakula duniani, nk.

2. Malengo ya Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu:
Lengo kuu la Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 ni kuiwezesha Tanzania kufikia kiwango cha maisha bora ya watu wake. Vipengele muhimu vya ubora wa maisha ni pamoja na afya na elimu bora, chakula cha kutosha na makazi bora, mazingira bora, usawa wa kijinsia na usalama wa watu binafsi. Sera ina malengo ya kuelekeza ubunifu wa sera za kisekta, mikakati na mipango mingine inayohakikisha maendeleo ya watu. Malengo mahususi ya sera ya mwaka 2006 ni pamoja na:

i. Maendeleo endelevu na kuondoa umaskini;
ii. Kuongeza na kuboresha upatikanaji na ufikiaji wa huduma bora za kijamii;
iii. Kuwa na mgao sawa, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na maendeleo kwa wote; na
iv. Mpangilio mzuri baina ya idadi ya watu, matumizi ya rasilimali na mazingira.

3. Viashiria vya idadi ya watu:

Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya 2012 inaonesha maendeleo na mabadiliko ya viashiria vya idadi ya watu ambavyo ni vizazi, vifo na uhamiaji, hivyo kuwepo haja ya kufanya mapitio katika Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu 2006 ili kuendana na mabadiliko hayo.

Uchambuzi wa takwimu za awali za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 unaonesha viashiria vingi vya idadi ya watu na maendeleo vimebadilika hivyo kuhitajika sera na mikakati mipya ya kutekeleza mipango mbalimbali ya idadi ya watu na maendeleo.

Sera ya Idadi ya Taifa ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 iliandaliwa wakati Watanzania walikuwa wanakisiwa kuwa takiribani milioni 38. Hata hivyo, idadi ya Watanzania kulingana na Sensa ya Idadi ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonesha kuwa Tanzania ina jumla ya watu milioni 44,928,923 ambapo Tanzania bara ni 43,625,354 na Tanzania Visiwani ni watu 1,303,569.

Taarifa hizo zinaonesha kuwa idadi ya vifo vya akina mama na watoto vimepungua kutoka 529 mwaka 1990 hadi kufikia 454 mwaka 2010, kwa kila vizazi hai 100,000 (Tanzania Demographics and Health Survey 2010 (TDHS 2010), kasi ya ongezeko la watu imepungua kutoka asilimia 2.9 (kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002) hadi kufikia 2.7 kwa mwaka 2012.

Vile vile, kasi ya uhamiaji imeongezeka maradufu ambapo kumekuwepo na wimbi kubwa la watu kuhama kutoka vijijini kwenda mijini au kijiji kimoja kwenda kijiji kingine (rural–rural migration). Aidha, kumekuwepo na suala la uhamiaji kutoka nchi moja na kwenda nchi nyingine kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi, kijamii na hata kiusalama, hii inajitokeza sana katika maeneo yanayozunguka maziwa makuu.
Kutokana na mabadiliko haya Serikali inaona kuna haja ya kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 na Mkakati wake wa utekelezaji ili kuendana na mabadiliko hayo.

4. Mapitio ya sera:
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itafanya mapitio ya Sera hiyo ili kuendana na taarifa mpya ambazo zimepatikana baada ya kukamilika kwa sensa, mapitio yanatarajia kufanyika katika kipindi cha mwaka 2014/15.

Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu inalenga kuratibu na kuhusisha sera, mikakati na programu nyingine ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya watu na kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake.

Vile vile Sera ya Idadi ya Watu inatoa fursa na maelekezo kwa sera zingine za kisekta kuweka kipaumbele masuala ya idadi ya watu na maendeleo katika kupanga mipango ya kisekta. Katika mapitio hayo, tunatarajia Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu iweke msisitizo katika kupanga na kutekeleza masuala yafuatayo;

i) Ukosefu wa ajira kwa vijana, wanawake na makundi maalum;
ii) Elimu kwa kuzingatia ngazi zote (awali, msingi, sekondari, hadi elimu ya juu) kwa makundi yote ya jamii;

iii) Uwezeshaji kiuchumi kwa kuzingatia makundi yote katika jamii;
iv) Umiliki wa rasilimali ardhi – nini kifanyike katika kuhakikisha kuwa jamii inashiriki katika kumiliki ardhi/mgawanyiko wa rasilimali za nchi kwa kuzingatia idadi ya watu na makundi mbalimbali katika jamii;

v) Miundombinu kwa kuweka kipaumbele mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum, kuweka miundombinu rafiki katika kutunza mazingira na maendeleo ya binadam kwa ujumla;

vi) Maendeleo ya miji na vijiji;
vii) Afya ya uzazi kwa kuzingatia mila, desturi, taratibu, sheria na kanuni zilizopo – kuweka msisitizo wa elimu kwa wote kama moja ya mikakati ya kuboresha afya ya uzazi; na
viii) Kuimarisha haki za binadamu.

5. Hitimisho:
Kwa ujumla unapozungumzia maendeleo unazungumzia watu na hivyo, katika kupanga tunapanga kwa ajili ya watu; kujua wako wangapi, wako wapi, na wanafanya nini.








All the contents on this site are copyrighted ©.