Waziri mkuu wa Cape Verde akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 3 Aprili 2014 amekutana na kuzungumza na
Bwana Josè Maria Pereira Neves, Waziri mkuu wa Cape Verde, ambaye pia alipta fursa
ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa
ameambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje
na ushirikiano wa kimataifa.
Ujumbe kutoka Cape Verde umeridhia pia makubaliano
ya ushirikiano kati yake na Vatican, yanayotambua Kanisa Katoliki kisheria. Itakumbukwa
kwamba, makubaliano haya yalitiwa sahihi kunako tarehe 10 Juni 2013.
Bwana
Jorge Borges, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Cape Verde ameongoza ujumbe wa nchi
yake, wakati ujumbe wa Vatican uliongozwa na Askofu mkuu Dominique Mamberti. Itifaki
hii inaimarisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili. Kuanzia sasa Jumapili itakuwa ni
Siku ya Mapumziko kitaifa. Serikali italinda na kuhifadhi maeneo ya Ibada, ndoa inayofungwa
na Kanisa kwa sasa inatambuliwa kisheria. Shule, taasisi na vyuo vikuu vinatambuliwa
kisheria. Kanisa limepewa fursa ya kufundisha dini shuleni pamoja na kuendelea kutoa
huduma za kijamii kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni.
Pamoja na
mambo mengine, itifaki hii inaliwezesha Kanisa Katoliki nchini Cape Verde kutoa huduma
za kichungaji katika vikosi vya ulinzi na usalama, hospitalini pamoja na kushughulia
masuala ya kodi na mali ya Kanisa. Itifaki hii imeanza kutumika rasmi baada ya kuridhiwa
na pande zote mbili.