Mshikamano wa kidugu uwe ni dira na mwongozo wa ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon katika hotuba yake ya ufunguzi wakati
wa mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika huko Bruselles, tarehe 2 Aprili
2014 amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato unaopania kudumisha
amani na usalama; maendeleo ya uchumi na kijamii pamoja na kuibua mikakati ya maendeleo
endelevu kwa siku za usoni.
Kuna haja kwa viongozi wa Ulaya na Afrika kushirikiana
kwa pamoja katika mchakato wa kuwajengea uwezo wanawake; kukuza na kudumisha usawa
pamoja na kuwasikiliza vijana. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujemga uwezo wa
kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa wote sanjari na kupambana na udhibiti wa
athari za mabadiliko ya tabianchi kadiri ya mikakati iliyopangwa na Jumuiya ya Kimataifa.
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, uhamiaji na mikakati ya maendeleo endelevu ni kati
ya changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa sanjari na kuhakikisha kwamba,
haki msingi za binadamu zinalindwa na kuheshimiwa. Katika shughuli zote hizi, mshikamano
wa kidugu unapaswa kuwa ni dira na mwongozo wa Jumuiya ya Kimataifa, ili kulinda na
kudumisha utu na heshima ya kila binadamu.