Jengeni na kuimarisha misingi ya haki, amani na upatanisho, vita haina mashiko tena!
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, hivi karibuni
kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko alifanya hija ya kichungaji nchini Sudan ya
Kusini, ili kuonesha mshikamano wa upendo kutoka kwa Mama Kanisa wakati huu Wananchi
wa Sudan ya Kusini wanapokabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na vita ya kikabila
na machafuko ya kisiasa nchini humo. Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan imepelekea
zaidi ya watu 1000 kupoteza maisha yao na wengine zaidi 150, 000 kuyakimbia makazi
yao.
Akihojiwa
hivi karibuni, Kardinali Turkson anasema, hija hii ya kitume ni kielelezo cha mshikamano
wa dhati kati ya Kanisa la kiulimwengu na Kanisa mahalia. Kardinali Turkson, mwanzoni
alipanga pia kutembelea wananchi wa Jamhiri ya Afrika ya Kati, lakini haikuwezekana
kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake. Mashambulizi yanayoendelea huko Afrika
ya Kati yasichukuliwe kuwa ni vita kati ya Waislam na Wakristo, bali changamoto kwa
wananchi Barani Afrika kudumisha utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika
tofauti zao za kidini, kiimani, kikabila na kisiasa na pamoja walenge kutafuta ustawi,
mafao na maendeleo ya wengi.
Kwa miaka mingi Waislam na Wakristo wamekuwa
wakiishi kwa amani, utulivu na mapendo, lakini tabia ya misimamo mikali ya imani,
inapelekea misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa kuanza kuyumba
sehemu mbali mbali za Bara la Afrika. Kumbe, kuna haja ya kushikamana kwa pamoja ile
kujenga Jamii inayoheshimiana na kuthaminiana.
Akizungumzia kuhusu mashambulizi
yanayofanywa na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria, Kardinali Turkson
anabainisha kwamba, kadiri ya taarifa alizonazo kutoka kwa Maaskofu Katoliki nchini
Nigeria, tatizo la Boko Haram ni tete kwani linaungwa mkono na baadhi ya wanasiasa,
kuna chochoko choko za kidini zinazoona kwamba, utamaduni kutoka katika Nchi za Magharibi
ni haramu na kwamba, unapaswa kupingwa kwa nguvu zote sanjari na kukataa kuridhia
mfumo wa elimu kutoka katika Nchi za Magharibi.
Ni kweli kwamba, dini zinaweza
kuchangia katika ustawi na maendeleo ya wananchi, lakini si kwa njia ya mtutu wa bunduki.
Watu wanapaswa kutambua na kuheshimu mafundisho ya dini zao ili waweze kweli kuwa
ni wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho wa kweli. Waamini wa dini
mbali mbali wasikubali kutumiwa na wanasiasa kusababisha kinzani na vurugu kwa ajili
ya mafao ya wanasiasa hawa, kwani watakaoumia si wanasiasa bali wananchi wasiokuwa
na hatia.
Watu watambue kwamba, kwa njia ya mtutu wa bunduki hata kile kiwango
kidogo cha maendeleo kilichokuwa kimefikiwa kitaathirika, kumbe kuna haja ya kujenga
na kudumisha utamaduni wa majadiliano kama njia ya kutafuta suluhu ya migogoro ya
kisiasa, kijamii, kidini na kiuchumi. Watu wazungumze wakiongozwa na ukweli, haki
na mafao ya wengi.
Udini na Ukabila ni sumu ya maendeleo ya wengi, watu wasiendekeze
mambo haya, bali wawe ni wajenzi wa mshikamano wa kitaifa kwa kutambua kwamba, tofauti
zao si kwa bahati mbaya, bali ni mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wake. Viongozi
wa kisiasa na Kiserikali wajifunze kuheshimu Katiba ya Nchi ambayo kimsingi ni Sheria
Mama, kwani tatizo la kutaka kupindisha Katiba ndicho chanzo kikuu cha kinzani na
migogoro ya kisiasa, kijamii na kidini katika nchi mbali mbali Barani Afrika.
Inasikitisha
kuona kwamba, wakati wa kampeni za chaguzi nyingi Barani Afrika watu wanatumia kiasi
kikubwa cha fedha, kumbe wanaposhindwa katika uongozi, wanatafuta njia za mkato za
kutaka kuingia madarakani kwa nguvu, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha misingi ya
demokrasia na utawala wa sheria.
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la
Kipapa la haki na amani anasema, ujumbe mzito aliwaachia wananchi wa Sudan ya Kusini
ni matumaini yanayojengeka katika misingi ya usawa, uhuru wa kweli na udugu. Haya
ni mambo yanayohitaji muda mrefu ili kuweza kumwilishwa katika uhalisia wa maisha
ya wananchi wa Sudan ya Kusini.
Ni matumaini yatakayowawezesha kuwa na maisha
yenye furaha, amani na utulivu, kila mwananchi akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu
wake ndani ya Jamii husika. Watu wajifunze kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu
na kamwe wasitazamane kama adui. Serikali zitekeleze dhamana na wajibu wake wa kulinda
utawala wa sheria, amani, utulivu na maendeleo ya wengi.
Imeandaliwa na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.