2014-04-03 11:28:12

Haitoshi tu kuridhia mkataba wa kudhibiti silaha, bali utekelezaji wake!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni limepongeza hatua ya nchi tano zenye viwanda vikubwa vya kutengeneza na kuuza silaha duniani kwa kuamua kuridhia Mkataba wa Silaha wa Umoja wa Mataifa, biashara ambayo inayafaidisha sana makampuni ya silaha kutoka katika nchi za: Ufaransa, Ujerumani, Italia, Hispania na Uingereza. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, biashara ya silaha inadhibitiwa kwani ni chanzo kikuu cha maafa sehemu mbali mbali za dunia.

Pongezi hizi zimetolewa na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, siku ya Jumatano tarehe 2 Aprili 2014. Hadi sasa kuna jumla ya nchi 31 wanachama wa Umoja wa Mataifa zimekwisha ridhia mkataba huu na bado nchi 50 ambazo zikiridhia mataba unakuwa ni sheria. Hii ni changamoto kwa mataifa yaliyobakia kuhakikisha kwamba, yanaridhia Mkataba huu ili kulinda na kudumisha misingi ya amani na utulivu, kuliko kutafuta na kukumbatia faida kubwa inayotokana na biashara ya silaha, lakini inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya kuhamasisha nchi mbali mbali kuridhia mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha duniani hasa katika maeneo ambao vita imekuwa ni "chakula chao cha kila siku". Biashara ya silaha imepelekea ukiukwaji wa haki msingi za binadamu, vita na kinzani za kijamii Barani Afrika.

Serikali ya Marekani, Russia na China zinapaswa kuiga mfano kutoka katika nchi nyingine kwa kuridhia mkataba huu anasema Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Ikiwa kweli nchi mbali mbali za Umoja wa Mataifa zitaonesha utashi wa kisiasa kwa kuridhia na kutekeleza mkataba wa udhibiti wa silaha, basi, dunia inaweza kupata nafuu katika amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.