2014-03-31 08:41:56

Eti, mwanadamu ametamadunisha maisha ya dhambi!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, karibu tukitegee sikio kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani. Pamoja na utajiri wa mafundisho ya Mama Kanisa, ambayo anatulisha kwa wakati huu wa Mfungo wa Kwaresma, kwa namna ya pekee tutafakari juu ya maisha ya dhambi na hali yetu ya udhambi. RealAudioMP3

Kama tufundishwavyo ‘dhambi zetu ndizo hututenga na Mungu wetu’, tunataka kwa juhudi ya akili, utashi, mwili na roho, tujibidishe kuikwepa dhambi ili tuwe karibu na mungu wetu na pia karibu na jirani zetu, na zaidi tena tuwe na amani na nafsi zetu sisi wenyewe. Dhambi huharibu uhusiano wetu na Mungu, huharibu uhusiano-mwafaka na wanadamu wenzetu, na zaidi tena dhambi hufitanisha nafsi ya mtu hadi anajichukia mwenyewe.

Dhambi hiyo ni nini? Kwa tafanusi nyepesi na kwa mwangwi wa mafundisho ya imani yetu, tunaielewa dhambi kama tendo la akili na utashi la kwenda kinyume na amri/maadilisho ya Mungu, Kanisa na miongozo safi ya jamii zetu. Na tuna namna nyingi za kuichambua dhambi katika uhalisia wake. Kwa leo, tusikie aina mbili tu za dhambi.

Kwanza ni dhambi binafsi, ambayo ni jumla ya matendo maovu ambayo mtu binafsi hutenda kwa kujua na kutaka (Hiyo dhambi binafsi hudhihirika kwa mtu binafsi katika mawazo, maneno, matendo na kutokutimiza wajibu). Mtu anapoamua kuhaini amri za Mungu, amri za Kanisa au kuikorofi mifumo sahihi ya jamii adili, hapo anafanya dhambi binafsi. Anaziwajibikia yeye mwenyewe.

Na pili kuna dhambi jamii. Hii ni jumla ya mambo yote kinyume na mpango wa Mungu, ambayo jamii nzima au kundi fulani la watu huyafanya. Na kwa vile matendo hayo maovu huyafanya mara nyingi na hufanywa na wengi, kwa nje huonekana kama ndio utaratibu sahihi wa maisha. Hapo tusisitize kwamba dhambi-jamii, ni uhalalishaji wa mifumo-dhambi kama ndio taratibu adili za maisha. Kwa mfano, tunapoendekeza rushwa, mauaji ya aina zote, uzembe kazini (kutokutimiza wajibu), wizi wa mali ya umma,uendekezwaji wa mifumo jike na mifumo dume, kutojali utu, kutamadunisha uvivu, umasikini na ujinga nk. Mambo hayo kwa vile yanatendwa na wengi tena mara nyingi, kuna kishawishi cha kuona kuwa ndiyo utaratibu unaotakiwa.

Katika kipindi hiki cha Kwaresma, sisi (kila mmoja kwa dhamiri yake na kama jamii pia) tunatafakari pia juu ya dhambi zetu. Tunataka kwa dhati kabisa kujidhamirisha upya, ili tuweze kuona ubaya wa dhambi na matokeo yake. Pia tunataka kuomba neema ya kuwa na aibu takatifu; tuiogope dhambi, tuogope kutenda dhambi, tuwe na hofu ya mungu, tuwe na woga mwema.

Nyakati zetu hizi, inashuhudiwa hali isiyo ya kawaida!. Kuna ushetanishwaji wa hali ya juu wa jamii ya mwanadamu. Wanadamu tumekuwa watenda dhambi hodari, kwa sababu tunamhusisha shetani na mifumo yake itawale maisha yetu. Tunatenda dhambi kwa ujasiri na waziwazi, kana kwamba kutenda dhambi ni haki yetu. Tumetamadunisha maisha ya dhambi. Tumeua kabisa dhamiri ya dhambi, ndiyo maana tunashuhudia kwamba mahali pengi mifumo ya dhambi inalindwa, inatetewa na hata kujengewa hoja kwa gharama kubwa sana.

Tumemruhusu mwovu atawale akili zetu, mioyo yetu, familia zetu, kazi zetu na maisha yetu yote. Tunapoendekeza maisha ya dhambi, iwe ni binafsi au jamii, tunamtukuza mwovu na hivyo tunajiweka kuwa mali yake. Leo hii tutashuhudia kwamba, mtu aliye mdhambi hodari sana, hupata wafuasi wengi na mtu mwadilifu hupingwa na kuteswa vikali. Hayo ni matokeo ya mifumo-shetani ya maisha. Turudi kwa Baba mwenye huruma, anatungoja.

Tufanye nini tupate kurudi? Yule mwana mpotevu, alipojikuta akitaabika kwa matokeo ya dhambi yake, alizingatia moyoni mwake, akaamua kurudi kwa baba yake, kwenda kutubu (yaani kuanza upya mahusiano mema na familia yake aliyoiasi kwa dhambi) Alirudi nyumbani kujitafutia amani na usalama.

Na sisi watu wa leo tulisikie neno hilo. Hali ya dhambi ambamo leo familia ya mwanadamu inaogelea, inatupeleka wapi?? Leo kwa vile tumepoteza dhamira ya dhambi, tunaipondaponda jamii ya mwanadamu kwa kujiwekea mifumo hatarishi kwa utu wa mwanadamu na heshima ya jamii. Dhambi zinatutafuna kwa kujua na kutaka. Mpaka lini?? Na kibaya zaidi sisi kama jamii ya sasa, kuna mifumo-dhambi ambayo tunaiweka leo, itakayokuja kuwaangamiza watoto wetu na vizazi vyote baadaye. Tuamue sasa! Tuondoke, turudi nyumbani kwa baba tukatubu. Yaani turudi kwenye misingi ya utu wetu, sisi ni mali ya Mungu.

Mpendwa msikilizaji, tunaomba na kusihi sana, katika familia zetu, watoto wetu wafundishwe ubaya wa dhambi na matokeo yake. Wadhamirishwe juu ya hofu ya Mungu. Ni bahati mbaya sana katika Kanisa la Nyumbani leo, sisi watu wazima ndiyo tunaowafundisha watoto kutenda dhambi. Na wakati mwingine wanaiga moja kwa moja kwa kuona matendo yetu maovu. Katika familia zetu, kama kumejaa mapigano, matusi, wizi na kila aina ya uzembe, imani potofu na kila aina ya ushetani, mtoto atajifunza nini? Tukumbuke kwamba, familia ni shule ya maadili mema. Mtoto akijifunza uadilifu kutoka katika familia yake, atakua huku ajijengeka katika dhamiri njema. Akiharibiwa katika familia yake, ni ngumu kurekebishwa ukubwani. Dhambi, huuma, huharibu, huua na huangamiza kabisa.

Mara nyingi tunatenda dhambi kwa namna tofauti, na madhara yake tunayaona na tunateswa haswa. Na dhambi nyingine tulizofanya tunasubiri madhara yake. Tufanye nini basi? Dawa ya dhambi ni nini? Ni: TOBA , MSAMAHA na KUJIREKEBISHA, tunu ambazo tutazitafakari kipindi kijacho.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni Mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.