2014-03-31 15:30:35

Binadamu wote wanaalikwa kuutafuta mwanga wa Kristu.


(Vatican Radio) Jumapili wakati wa sala ya Malaika Bwana , akihutubia maelfu ya mahujaji na wageni, Papa Francisiko alisisitiza kwamba, binadamu wote wamealikwa kujifunua na kuusadiki mwanga wa Kristo, unao wezesha kuzaa matunda bora katika maisha. Na alionya dhidi ya upofu wa kiroho, wenye kuongoza katika matendo yaliyo kinyume na Injili. Kiini cha ujumbe wa Papa, hasa kililenga katika somo na Injili ya Jumapili ambamo Mtume Yohana anaeleza juu ya muujiza wa kuponywa kwa mtu kipofu tangu kuzaliwa, aliyeponywa na Yesu.

Papa aliendelea kufafanua kwamba, Mtume Yohana anaeleza tukio hili si kwa nia ya kuonyesha muujiza uliofanywa na Yesu lakini hasa kile kilichofanyika baada ya tukio. Alisema, kulianzishwa minong’ono mingi, kati ya wale wanaosadiki na wasiosadiki, kama ilivyo kawaida , kwa matukio mengi, huleta minong’ono, wengi wakitaka kujionea wenyewe au kujua ukweli. Na ndivyo ilivyokuwa wakati wa tukio hili la Kipofu kuponywa na Yesu. Wengi walitaka kuhakikisha kilichotokea.

Papa alisema, Mtume Yohana , alimlinganisha mtu huyo kipofu tangu kuzaliwa ambaye macho yake yanarejeshwa na wale ambao licha ya macho yao ya kimwili kuona, wanaupofu wa upofu wa kiroho, kwa kuwa tangu kuzaliwa, hawajakutana na Injili. Bado kumulikiwa na mwanga neema ya Kristo. Watu ambao wakiisikia Injili, habari njema ya wokovu unaoletwa na Yesu , huamini na kuongoka, na hivyo kuwa tofauti walimu wa sheria, ambao wanaijua sheria lakini wanaendelea kutosadiki na kubaki na upofu wa kiroho. Na kwa kiburi chao walimu hao, licha ya kuwa na Yesu, waliendelea kutosadiki na hivyo walibaki wameifungia nje neema ya wokovu , kwa imani kwamba ayari wanao mwanga na kukataa kusadiki ukweli wa Yesu. Walimu hao, alifanya kila lililowezekana kuukataa ushahidi wote. Na hata walishakia utambulisho wa mtu kipofu aliyeponywa na Yesu. Walishakia utendaji wa Mungu wa kuponya ,kwa kisingizio kwamba Mungu haponyi siku ya Sabato.
Baba Mtakatifu alibaini, wakati mwingine maisha yetu , ni kama ya yule mtu kipofu, tunakiri na kuusadiki mwanga wa Injili ya Kristo na kuponywa kiroho. Lakini, wakati mwingine , kwa bahati mbaya , alisema , pia ni kama wale walimu wa Sheria, tunakataa kusadiki ushuhuda unaotolewa, tunaweka mashaka katika utendaji wa Mungu na kuhukumu ya wengine.
Lakini Papa Francis alisisitiza, sisi sote tumealikwa kusadiki ukuu wa Mungu na utendaji wake unaofanikishwa na mwanga wa Kristo, wenye kuwezesha kuzaa matunda boya katika maisha yetu. Kuondokana na tabia zisizo kuwa na utambulisho wa Mkristo ,na kutembea imara katika njia ya utakatifu. Papa ametoa mwaliko kwa waamini kurudia tena kuisoma kwa makini, sura hii ya Injili ya Yohana , na kuipima dhamiri, iwepo kweli tumejifunua wazi kwa Mungu na jirani .

Baada ya hotuba yake kama kawaida Papa alitaja baadhi ya makundi yaliyokuwa yamekusanyika katika uwanja huu wa Mtakatifu Petro, wakiwemo wanajeshi wa Italia, ambayo walikuwa wanahitimisha hija yao kwa kutembea kwa miguu kutoka Loreto hadi Roma, kwa ajili ya kuomba amani na utatuzi wa migogoro ya kisiasa katika taifa lao . Papa aliwashukuru kwa juhudi hizi, akisema, ni vyema sana kufanya hivyo, kama ilivyoandikwa katika Heri Nane, heri wale wanaofanya kazi kwa ajili ya amani.








All the contents on this site are copyrighted ©.