Ninatumaini sisi sote tumewahi kuusikia msemo huu: “Funguka macho, Angalia!” Usemi
huu hauna maana kwamba mmoja ni kipofu au amefumba macho yake na sasa anaambiwa ayafungue
ili aweze kuona, la hasha bali ni “Kufungua Macho” ili kuweza kuona vyema mambo katika
maisha. Mathalani, neno hili linaweza kutumika na wazazi wanaomwonya mtoto wao wa
kike anayempenda mvulana mwenye matatizo labda ya kubugia unga, au wizi au hana maisha
mazuri au mvivu na hataki kufanya kazi.
Mama mtu anaweza kumwangalisha bintiye
na kumwambia: “Mwanangu, funguka macho. Je, huioni hali halisi ya maisha ya huyo kijana
unayempenda? Angalia sana usije ukajitatiza. Utadhani umepata kumbe umepatikana!”
Kwa hiyo, kuna upofu unaotibiwa hospitalini na mganga wa macho, lakini pia kuna upofu
mkubwa unaokupotezea mwelekeo wa maisha, upofu unaokuzuia usiweze kuona hatari iliyo
mbele unakoenda katika maisha, upofu ambao unakufanya usione na kuchukua uamuzi gani
unaofaa wa kufuata. Maisha kwako yanakuwa giza. Unabaki kama kipofu unayeegemea ukuta,
au mkongojo, au kuwategemea wazazi. Wakati kumbe mtu anayeona ni huru hamtegemei mtu
yeyote yule.
Leo tutapambana na mganga mkuu wa tiba ya upofu wa macho wa aina
hii ya pili. Tutapata mwongozo wa kujikwamua na upofu wa maisha kijumla. Mwinjili
Yohane anatuletea kituko cha uponyi wa kipofu wa macho kwa namna kama ya tamthilia
au mchezo wa kuigiza ili kutufafanulia vizuri maana ya upofu huo wa maisha na uponywaji
unaofanywa na Yesu.
Yesu anajionesha kama mganga wa macho, mponyi wa upofu
unaotuwezesha kuona vyema njia tunayosafiri katika maisha na kuchagua vyema maisha
kadiri ya thamani zitakiwazo. Kuna usemi wa Yesu anaosema: “Pindi niko duniani, mimi
ni mwanga wa ulimwengu. Yesu ni jua linalomeremeta na kutuangaza sote.” Kutokana na
ukweli huo, Injili ya Yohane inafungua kwa neno hilo la mwanga: “Kulikuja nuru amtiaye
nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Yohane mbatizaji hakuwa nuru, bali alikuja
kuishuhudia tu ile nuru yenyewe.” (Yoh 1:7-9).
Kristo ni mwanga unaotuwezesha
kuona vyema maisha kwa namna inayoipa maana ya maisha yetu. Injili hii daima ilikuwa
inatumika jumapili ya leo katika safari ya wakatekumeni watakaobatizwa Jumamosi Kuu.
Baada ya kuibuka toka kwenye kisima cha ubatizo wakawa wanaitwa walioangazwa, wanaomeremeta.
Yaani wale waliokuwa wamepata zawadi ya mwanga toka kwa Kristu! Waliofunguliwa macho
juu ya kuuona vizuri ulimwengu.
Yawezekana kabla yake walikuwa wevi, wadanganyifu,
wachakachuaji, wala rushwa, lakini bila kujitambua kuwa ni vipofu wakapotea njia,
wakawa wanapuyanga porini tu hata hawajui wanakoelekea. Sasa wanafuata Injili ya Kristo
inayowafungua macho yao. Hali ambayo tunaweza kuipata hata sisi, tunapokosea, kufanya
uchaguzi usiofaa katika maisha, anafika mmoja na kutufungua macho, anapotuambia “Angalia,
Kaa chonjo, Jihadhari,” hapo tunashtuka kwani tungekosea halafu mapato yake yangekuwa
mabaya. Huo ndiyo ufunguo wa kuelewa fasuli ya Injili ya leo.
“Yesu alipokuwa
anapita alimwona kipofu tangu kuzaliwa.” Hatuambiwi jina la mtu huyo, bali anatajwa
tu kuwa ni kipofu, anaweza kuwa mtu yeyote yule. Maana yake hiyo ni hali ya kibinadamu,
ya mtu yule ambaye hajakutana na Yesu, amezaliwa kipofu. Mtu wa namna hiyo, hawezi
hata kuhitaji mwanga au nuru, kwa sababu haufahamu ulivyo kwa sababu hajauona. Wakati
mwingine tunaweza kusikia watu wakisema: Mume wangu haendi kabisa Kanisani kusali,
na hana hata wazo la kusoma biblia au kusikiliza mazungumzo ya mambo ya dini. Au unakutana
na mtu, anakuambia “mimi sina hamu kabisa na ukristo, yaani sina interest kabisa!”
Hilo si jambo la kushangaza, kwa sababu Mtu ambaye hajauona mwanga, (kipofu)
hajakutana na Kristu, itakuwa ni kumdai mno mtu wa namna hiyo (kipofu) atamani kuutazama
ulimwengu kwa namna tofauti. Kwa sababu hana wazo, hawezi kufikiri namna nyingine,
hawezi kujua, ni kitu gani hiyo nuru. Mtu aina hiyo ni kipofu anahitaji kufunguka
macho. Ni sawa na mtu anayekuja kugundua uhondo wa muziki, uhondo wa riadha, uhondo
wa kufanya hija, uhondo wa kusoma hesabu, uhondo wa siasa, nk. Kabla yake hakuwa anashabikia
chochote, sasa utamkuta anafurahia kwa sababu kuna mtu amemfungua macho – anakuwa
limbukeni hana siri.”
Wanafunzi wa Yesu wanapomwona huyo kipofu wanakuwa kama
waafrika mbele ya matatizo, wanaanza kumtafuta mchawi, wanamwuliza Yesu: “Rabi, ni
yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?” Hebu angalia
kwa makini jibu la Yesu ni tofauti kabisa na fikra zetu. Anajibu kifupi tu: Hiyo ni
hali halisi ya maisha. Kwamba mtu anazaliwa hivyo. “Hiyo ni kazi ya Mungu.” Mwanga
huu unatoka mbinguni, siyo jambo analoweza kulileta binadamu. Yawezekana akaendelea
kuwa kipofu hivyo hadi kufa, au kuweza kubahatika kukutana na Kristu anayeweza kukufungua
macho kwa neno lake.
Yesu hataki kusikia watu wanazungumza juu ya dhambi kama
inavyozoeleka kusikia kwamba, dhambi imeingia duniani kwa njia ya wazazi wetu wa kwanza
na hivi sisi sote tuko katika dhambi, la hasha, bali sisi tunazaliwa hivyo. Yesu anatualika
kufunguka macho, kuangalia nuru ya Mungu daima, na ni yeye pekee anayeweza kutufungua
macho na kuona ulimwengu kwa namna ya pekee.“Baada ya kusema hayo, Yesu alitema mate
chini na kufanya tope kwa yale mate. Kisha akampaka kipofu kope za macho”. Tendo hilo
ni muhimu sana, kwa vile inarudiwa kusemwa mara tano katika fasuli ya Injili ya leo
Yesu alitema mate chini na kufanya tope kwa yale mate.
Tumeshasikia mara nyingi
katika Agano la kale, juu ya tope, ya pumzi ya Mungu na mate. Hayo yanamaanisha uhai
au uzima. Kitendo kilichofanyika cha Mungu alipomwumba Adamu. Yesu anakirudia kitendo
hicho ikiwa kama ni uumbaji upya wa mtu mpya. Sasa mtu mpya anazaliwa kutokana na
mwanga wa Kristu. Yaani sasa mtu anaishi kama inavyotakiwa kuwa binadamu. Anajua anakotakiwa
kwenda kisha anamtuma huyo kipofu na kumwambia: “Nenda kanawe katika birika ya Siloamu,
maana yake aliyetumwa.” Wataalamu wanasema Siloamu maana yake siyo aliyetumwa, neno
kutumwa lingekuwa shaluak ambacho ni kisima pekee kilichokuwa katika mji ule
wa Yerusalemu.
Hapa kwa neno hilo mwinjili anataka kuonesha maji yale ambayo
yanamfungua macho, kama maji ya ubatizo, na yule ambaye anampa mwongozo wa kuyapata
hayo maji yaani Roho wa Kristu, yaani maisha ya kimungu ambayo yanakuwezesha kuona
hali halisi ya maisha. Baada ya kutoka kisimani kunafuata mfululizo wa vituko vinavyomsibu
kipofu huyu aliyepona. Hiyo ni sawa na safari ya mtu anayeona mwanga baada ya kufunguliwa
macho na Yesu. Mtu anayesafiri peke yake bila kutegemezwa na Yesu. Safari ya kipofu
huyu ni sawasawa na safari yetu wakristu kuelekea mwanga. Unaalikwa kutanguzana kipofu
huyu ujifunze kutembea vyema baada ya kupata mwanga wa ubatizo ili kuelekea kwenye
mwanga halisi wa maisha.
Kulikuwa makundi kadhaa ya watu waliokuwa wanahoji
na kuujadili uponyi wa kipofu huyu kwa namna yao. Kikundi cha kwanza alichopambana
nacho huyu kipofu ambaye sasa anaona ni cha majirani waliokuwa karibu sana naye: Watu
hao wanaonekana sasa kutokuwa na uhakika kama wanayemwona ndiye aliyekuwa kipofu mwombayala
maskini au la, wanaulizana: “Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba? Wengine
wakasema ndiye. Wengine wakasema, La! lakini amefanana naye.”
Tunaweza kujiuliza,
je, kumetokea nini hadi Mtu huyu hatambulikani tena na jirani zake alioishi nao. Hiyo
ndiyo historia ya maisha yetu, hiyo ni hali halisi ya maisha yetu. Historia ya wale
waliokuwa vipofu ambao walikuwa wanatembea bila kuelewa wachukua uchaguzi gani mzuri
wa maisha. Wanapofunguka macho katika nuru ya Kristu, wanakuwa watu tofauti kabisa
hadi kutokutambulikana tena na watu aliozoeana nao kabla.
Yawezekana mtu alikuwa
anathamini mambo mengine kabisa ya duniani, magari, nyumba, raharaha, lakini sasa
amegundua thamani nyingine bora zaidi za maisha. Labda alikuwa mpiga rushwa, au mchakachuaji,
mdanganyifu, sasa ni kinyume chake. Sasa amefunguka macho. Hivi unapokutana na wanaomfahamu,
wanaweza kubishana wenyewe kwa wenyewe. Ni yule au siyo yule tunayemfahamu? Maana
yake mtu aliyeangazwa kweli, anakuwa tofauti kabisa kwa sababu yuko katika safari
kuelekea mwanga.
Wanapomwuliza Kipofu huyo anathibitisha kwamba ndiye: “Mimi
ndiye”. Watu hao wanataka kujua “Kulikoni” wanamwuliza “Yalifumbukaje”. Naye anarudia
kueleza ilivyokuwa: Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope akanipaka macho akaniambia,
Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona”. Inakuwa vizuri sasa
hata mimi ninapoulizwa swali la mtindo kama huo imekuwaje hadi uwe mkristu, ulipatapataje
wito wa ukristo, wa utawa, wa ukatekista au upadre?
Kipofu anaendelea na safari
yake ya maisha. Mara anakutana na kikundi cha pili cha watu ambao ni viongozi wa kanisa.
Yaani watunzao mapokeo yadini na ambao tungetegemea wangestaajabia kumwona aliyekuwa
kipofu sasa anaona. Kumbe hao wanachukizwa na mtu aliyemfungua macho kipofu huyu.
Kikundi hicho cha pili siyo cha wengine bali ni cha Mafarisayo: Chuki yao inakuja
pale wanapotambua kwamba, huyu kipofu kabla yake alikuwa anafuata amri zao, alikuwa
anafanya wanachotaka wao, alikuwa amewategemea kumbe sasa amefunguka macho, anaona
mambo kwa namna tofauti.
Hao ni maadui wa nuru, wanawawakilisha wale walio
wafungwa wa fikra zao, dhana zao, mawazo yao juu ya Mungu. Wamefungwa katika utamaduni
na mapokeo yao na hawataki kubadili kitu. Hapo wanasema mtu aliyemponya kipofu siyo
mtu wa Mungu kwani hashiki sheria ya sabato ya mapokeo yetu. Hivi wanamhoji: “Mafarisayo
nao wakamwuliza tena jinsi gani alivyopata kuona.” Naye kipofu anatoa majibu yaleyale
aliyotoa mwanzoni: “Alinitia tope juu ya macho nami nikanawa, na sasa naona.” Wanapobishana
wao kwa wao juu ya mtu huyo wanagawanyika na wanashindwa kupata jibu wanalolitaka,
wanamwuliza tena kipofu mara ya pili, “Wewe wasemaje katika habari zake kwa vile alivyokufumbua
macho?” Kipofu anatoa jibu linalompa cheo zaidi Yesu: “Mimi kwa binafsi yangu naona
kuwa mtu huyu: ‘ni nabii’”.
Kikundi cha tatu ni wazazi wanaoitwa na wafarisayo
na kuulizwa maswali: Wazazi wanamfahamu vizuri sana mtoto wao. Viongozi wanawauliza
wazazi “Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje,
basi kuona?” Wazazi wanaruka swali la pili na kulijibu la kwanza: “Tunajua ya kuwa
huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu; lakini jinsi aonavyo sasa hatujui.
Wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Sisi hatumo katika suala la kufunguka kwake
macho. - Mwulizeni yeye mwenyewe, yeye ni mtu mzima, atajisemea mwenyewe.” Yaani alizaliwa
kipofu, na kuna mwingine amemfungua macho”.
Hapa unaona kama vile wazazi hawa
wanaogopa, wana woga wa kuponywa. Wanamwogopa kijana anayeona mambo kwa namna ya pekee
kuliko namna ile waliyomfundisha wao. Wazazi wana wasiwasi, kwa sababu wale ambao
hawafuati mapokeo wanaweza kufukuzwa toka hekaluni. Hapa unaweza kuwakumbuka watu
ambao wametoa mchango mkubwa sana katika jamii, katika siasa lakini hawapokewi vizuri.
Mwanga ni hatari, unagombanisha watu.
Kinakuja kikundi kingine cha nne ambacho
ni kilekile tena cha mafarisayo, wanamwambia yule kipofu: “Mpe utukufu Mungu.” Ni
sawa na kusema: “Umshukuru Mungu”. Maana yake, wewe kiri tu kwamba umekosea, kisha
sisi tutajitahidi kuweka mambo sawa. Hasahasa kurekebisha kufuru hii iliyojitokeza
kwa sababu “Sisi tunajua ya kuwa mtu huyo ni mwenye dhambi.”
Hapo kipofu anaanza
kuitetea hali halisi anayojisikia kuwa nayo, yaani hali ya kuona mwanga mpya wa Kristu
aliyemfungua macho hayo. Anawapa ukweli wao: “Kwamba yeye ni mwenye dhambi hilo mimi
silijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona.” Hapo tunajifunza
kwamba yabidi kwa haki yote kujiacha kutetewa na matendo na siyo kwa sheria. Unaona
wazi kuwa mtu huyu aliyepata mwanga sasa anazidi kuwa na uhakika zaidi wa mambo na
kujiamini zaidi.
Wanapomwulizia tena jinsi alivyofumbuka macho wanapomwuliza:
“Alikutendea nini? Alikufumbua macho jinsi gani?” Wanataka aendelee kujibu, ili waweze
kutafuta mwanya wa kumkosoa. Hapo yule kipofu anawashtukia na kuwapa “makavu laivu”.
“Nimekwisha kuwaambia, wala hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena? Yawezekana labda
na ninyi mnataka kuwa wanafunzi wake?” Ni kitu cha kawaida kutoa majibu haya makavu.
Na kutoka hatua hii sasa wanaanza kutupiana lugha za kebehi na matusi ya rejareja.
“Wewe ndiye mwanafunzi wake, sisi tu wanafunzi wa Musa. Sisi tunajua ya kuwa Mungu
alisema na Musa; bali yule hatujui anakotoka.” Mafarisayo daima wanakimbilia kusema:
“Sisi tunajua” na huyu kipofu daima anasema “Mimi sijui”. Watu wanaofikiri kwamba
daima wanajua yote hawawezi kupata mwanga, watabaki daima kuwa katika giza.
Wafarisayo
wanaposema kwamba hawajui anakotoka Yesu, kipofu anawakebehi tena na kuwaambia: “Hii
ni ajabu! Ninyi mnaojua mambo yote, lakini hamumjui anakotoka huyu aliyenifumbua macho!”
Ni kama anawaambia: “Tunakichojua sisi wenyeji yaani watu wa kawaida ni hiki kwamba,
mcha Mungu (anayemwogopa Mungu) daima anasikilizwa na naye Mungu.
Aidha, haijawai
kusikika kwamba kumetokea mtu anayafumbua macho ya mtu aliyezaliwa na hali ya kipofu.
Asiyetoka kwa Mungu hawezi kutenda neno lolote.” Kutoka kwenye hali ya kebehi hadi
wanafikia kukashifiana na kutoleana lugha chafu. Hawa wafarisayo, wanashindwa kuhimili
vishindo wanaamua kumfukuzia nje. Ni namna dhahiri ya kutenda ya mtu asiyetaka kufunguka
macho na kuuona mwanga. Ukifuatilia mazungumzo haya utaona jinsi yalivyopanuka kidogokidogo
kutoka kwenye ushawishi, kebehi na dharau matusi hadi kuchefuana nyongo na mwisho
kumfukuza mtu. Ndiyo mtindo wa kufanya mambo mtu asiyetaka kufunguka macho. Kipofu
anaondoka, anajiona kuwa huru anatoka nje.
Katika sehemu ya mwisho ya Injili
tunasikia kwamba yule kipofu akakutana tena na Yesu. Lakini ukweli ni kwamba Yesu
alimtafuta yule kipofu ndipo walipokutana nje walikofukuziwa wote wawili. Yesu anaenda
kumtafuta mwenzake ambaye naye amefukuzwa kama yeye. Anajua kuwa yule anayepokea mwanga,
hawezi kutazamwa vyema na watu wa mapokeo. Yesu akamwuliza: “Wewe wamwamini Mwana
wa Mungu?” Yaani wewe unajiaminisha kweli kwa mtu aliyekufungua macho? Yule kipofu
anajibu “Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?”. Yesu anamjibu: “Umemwona, unayesema naye
ndiye.” Mtu aliyeangazwa hahitaji tena uwepo wa mwalimu. Alikuwa ameongozwa katika
safari yake na ile Injili inayoendelea kumfungua macho. Ndugu yangu, katika safari
yako ya maisha funguka macho uongozwe na nuru ya Kristo yaani Neno lake. Alcuin
Nyirenda, OSB.